
Katibu kutoka Serikali ya Ujerumani, Jochen Flasbarth (katikati) akifurahi kuzindua zahanati mpya ya kisasa katika kijiji cha Bokore wilayani Serengeti leo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Kemirembe Lwota, miongoni mwa viongozi wengine.
---------------------------------------
Ni matunda ya uhifadhi. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya uzinduzi wa miradi minne ya kijamii iliyogharimu mamilioni ya fedha katika vijiji mbalimbali vilivyopo wilaya za Serengeti, mkoani Mara na Ngorongoro, mkoani Arusha.
Miradi hiyo ambayo imetekelezwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na Shirika la Uhifadhi ya Kimataifa la Frankfurt Zoological Society (FZS) chini ya ufadhili wa Serekali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), imezinduliwa rasmi jana Jumamosi na leo Jumapili.
Miradi iliyozinduliwa kwa upande wa wilaya ya Serengeti ni barabara mpya ya Park Nyigoti-Nyichoka iliyojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.3, na zahanati ya kisasa katika kijiji jirani cha Bokore ambayo ujenzi wake umegharimu shilingi milioni 450.
Kwa upande wa Ngorongoro, miradi iliyozinduliwa ni vyumba vitatu vya madarasa, ofisi ya walimu na vyoo vyenye matundi saba kwa ajili ya wasichana katika Shule ya Msingi Sukenya iliyogharimu takriban shilingi milioni 200, na barabara ya Soitsambu-Kritalo yenye urefu wa kilomita 12.5 iliyogharimu shilingi biloni 1.1.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo, Katibu kutoka Serikali ya Ujerumani, Jochen Flasbarth ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo ambayo inalenga kuboresha maisha ya maelfu ya wananchi wanaoishi jirani na ikolojia ya Serengeti.
“Hii ni miradi mizuri sana,” amesema Flasbarth ambaye pia alifuatana na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Thomas Terstgen.

Katibu kutoka Serikali ya Ujerumani, Jochen Flasbarth (katikati) akikata utepe kuzindua barabara ya Soitsambu-Kritalo (kilomita 12.5) wilayani Ngorongoro, Arusha jana, iliyotekelezwa na TANAPA kwa kushirikiana na FZS chini ya ufadhili wa Serekali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW). (Picha zote na Sauti ya Mara)
------------------------------------------
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Kemirembe Lwota ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kufadhili miradi hiyo, na kuwataka wananchi husika kuilinda na kuitunza kwa manufaa yao.
DC Lwota pia amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi wa wanyamapori na mazingira.
“Haya maendeleo yote yanafanyika kwa sababu ya uhifadji, twendele kuhifadhi wanyamapori na kulinda mazingira,” amesema kiongozi huyo wakati wa uzinduzi wa zahanati ya Bukore.
Ameongeza kuwa misaada hiyo ni kielelezo cha matokeo chanya ya uhusinao mzuri uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Ujerumani.
Aidha, wananchi wa maeneo hayo wamesema miradi hiyo itasaidia kubadilisha maisha yao kuwa mazuri, na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za uhifadhi.
“Sisi tumenufaika sana kutokana na ujenzi wa hii barabara na zahanati, tunaishukuru Serikali ya Ujerumani na tutaendelea kuwa wahifadhi,” amesema Mwenyeki wa Serikali ya Kijiji cha Bokere, Nelson James.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Viongozi wa Afrika wakutana Tanzania kujadili kuhusu nishati
>>Barrick yazidi kung’ara mgodi wa North Mara ukitwaa tuzo kwa ulipaji bora wa kodi
>>NECTA yatangaza matokeo ya kidato cha nne 2024
>>Barrick North Mara yakabidhi bilioni 3.7/- za ‘service levy’ Tarime Vijijini, bilioni 1.7/- za mrabaha kwa vijiji vitano
No comments:
Post a Comment