
Mwenyekiti wa MRPC, Mugini Jacob akifungua semina ya uwekezaji kwa wanahabari mkoani Mara leo. Kulia ni CPA Boniface Ndengo, Mkurugenzi Mkuu wa HAIPPA PLC iliyoandaa semina hiyo, na kushoto ni mwaandishi wa habari Maximillian Ngessi.
------------------------------------
Kampuni ya HAIPPA PLC imezindua semina ya uwekezaji kwa waandishi wa habari nchini, kwa kuanza na baadhi ya waliopo mkoani Mara.
Semina hiyo imeendeshwa na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo ya umma, CPA Boniface Thomas Ndengo mjini Musoma leo Januari 28, 2025.
“Tumeanza na mkoa wa Mara lakini semina kama hii itafanyika nchi nzima,” amesema CPA Ndengo.
Washiriki wa semina hiyo wameelimishwa maana ya kampuni za umma, uanzishaji wake, ununuzi wa hisa kwenye kampuni hizo na faida zake.
CPA Ndengo akiwasilisha mada katika semina hiyo. (Picha zote na Mara Online News)
---------------------------------------
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa semina hiyo alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), Mugini Jacob Mwera ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa semina hiyo, Mugini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mara Online News na Gazeti la Sauti ya Mara, ameipongeza HAIPPA PLC kwa hatua kubwa iliyofikia.
Amewaomba waandishi wa habari kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza kampuni hiyo na faida zake katika jamii.
“Tuitangaze HAIPPA PLC ili tuwe sehemu ya mafanikio yake,” Mugini amewaomba waandishi wa habari na kuiahidi kampuni hiyo ushirikiano wa dhati kutoka MRPC.
Kwa mujibu wa CPA Ndengo, HAIPPA PLC ilianza na wanahisa wanane, na hadi sasa ina wanahisa 459 na imeshauza hisa 380,000.
Kaulimbiu ya semina hiyo inasema “Tuwawezeshe Watanzania Washiriki Uwekezaji Mkubwa”.
HAIPPA PLC ni Kampuni ya Umma iliyoanzishwa mwaka 2022. Ndoto yake ni kuwa shule bora ya uwekezaji Tanzania na Afrika.
Dhamira ya kampuni hiyo ni kubuni, kujenga, kuwekeza na kuwezesha miradi mikubwa Afrika.

Viongozi wa HAIPPA PLC, mgeni rasmi na waandishi wa habari walioshiriki semina hiyo wakifurahia picha ya pamoja.
Read Also Section Example
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Ajali ya ndege Marekani yaua watu 67 wakiwemo wanajeshi
>>Wasira kuanza ziara ya kukagua maendeleo ya CCM mkoani Mara leo
>>Sekondari ya Tarime Mchanganyiko yang’ara matokeo kidato cha nne 2024
>>Barrick North Mara yakabidhi bilioni 3.7/- za ‘service levy’ Tarime Vijijini, bilioni 1.7/- za mrabaha kwa vijiji vitano
No comments:
Post a Comment