
Muonekano wa Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko kutokea angani.
----------------------------------
Na Mwandishi Maalum/ Mara Online News
Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko imeandika historia mpya ya mafanikio, baada ya wanafunzi wake wote kupata ufaulu wa juu katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2024.
Wanafunzi wote 15 (wasichana 13 na wavulana wawili) waliofanya mtihani huo shuleni hapo wamepata ufaulu mzuri unaowapa uhakika wa kuchaguliwa kujiunga na kidato cha sita na vyuo vya kati mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Mwita Samson Marwa, wanafunzi wanne (wavulana wawili na wasichana wawili) wamepata ufaulu wa daraja la kwanza (division I), sita (wote wasichana) wamepata daraja la pili (division II) na watano (wote wasichana pia) wamepata daraja la tatu (division III).
Hivyo, hakuna mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko aliyepata daraja la nne (division IV) wala kufeli kwa kupata alama sifuri (division 0).

Mkuu wa Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko, Mwalimu Mwita Samson Marwa.
----------------------------------

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Tarime mchanganyiko, Mwalimu Janeth Joseph.
---------------------------------------
“Siri ya wanafunzi wetu kupata ufaulu mzuri katika mtihani huo, ni usimamizi makini, jitihada za walimu katika kujituma kufundisha na nidhamu ya wanafunzi wenyewe,” alisema Mwalimu Mwita katika mahojiano maalum na Sauti ya Mara mjini Tarime juzi.
Mwalimu Mwita ambaye pia ni Meneja Uendeshaji wa Taasisi ya Professor Mwera (PMF) inayomiliki shule hiyo, alifafanua kwamba wanafunzi hao walijengewa mazingira bora ya kusoma kwa bidii na kuwa tayari kushirikiana na walimu katika mahitaji yao muhimu.
Hata hivyo, alidokeza kwamba shauku kubwa ya uongozi wa shule hiyo ni kuona wanafunzi wake wote wanapata ufaulu wa daraja la kwanza (division I) katika mitihani ya taifa kuanzia mwaka huu na kuendelea.
“Tumejipanga vizuri ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wetu wote wanapata daraja la kwanza. Tunaomba wazazi na walezi waendelee kutuamini na kuleta watoto wengi wapate elimu bora katika sekondari yetu ya Tarime Mchanganyiko,” alisema Mwalimu Mwita.
Kwa upande wake mwanafunzi wa shule hiyo, Gasaya Kerato Nyanguru ambaye amepata ufaulu wa daraja la kwanza lenye alama saba, alisema bidii ya kusoma na mawasiliano mazuri na walimu vilimpa uhakika wa kupata mafanikio hayo.
“Nilitumia muda wangu mwingi kusoma na kuuliza walimu maswali ya kunisaidia kitaaluma,” alisema Gasaya ambaye anatamani kuwa daktari wa binadamu baada kuhitimu masomo.

Gasaya Kerato Nyanguru
---------------------------------
Gasaya alitumia nafasi ya mahojiano na Sauti ya Mara pia kutoa wito kuhamasisha wanafunzi wote kujituma kusoma kwa bidii na kuzingatia maelekezo ya walimu.
“Ninawapongeza walimu wa shule yangu ya Tarime Mchanganyiko na ninawaomba waendelee kuongeza jitihada za kufundisha ili kuiwezesha kupata matokeo mazuri zaidi katika mitihani ya kitaifa,” alisema Gasaya.
Aidha, Mwalimu Mwita na mwanafunzi huyo walitumia fursa hiyo pia kuwashukuru na kuwapongeza wazazi na walezi kwa ushirikiano mzuri wanaowapa katika jitihada za kuinua taaluma kwa wanafunzi katika shule hiyo.
Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko kwa sasa ina mkondo wa Amali (Ufundi) katika fani za ufundi magari, umeme, bomba, useremala, uchomeleaji vyuma, kushona na kudarizi, joninery, computer programming na graphics and design.
Shule hiyo ipo mjini Tarime mkoani Mara, na inamilikiwa na Taasisi ya Professor Mwera (PMF) ambayo ina kibali cha serikali cha kufanya kazi zake na mikoa yote nchini baada ya kufanya vizuri katika mikoa 10 ya awali.
“Baada ya kupewa kibali na Wizara ya TAMISEMI cha kufanya kazi zetu ndani ya mikoa 10, tuliaminiwa zaidi na kupewa kibali na wizara cha kufanya katika nchi nzima,” anasema Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera.
Kwa mujibu wa Hezbon, PMF imejikita zaidi katika kuhamasisha vijana kujiunga na vyuo vya ufundi wakati wanasubiri matokeo ya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na sita, na hata darasa la saba ili kupata stadi za ufundi zitakazowawezesha kujiajiri, au kuajiriwa, hivyo kuondokana na utegemezi katika familia na jamii kwa ujumla.

Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera.
---------------------------------
Hezbon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, anasema taasisi hiyo inatoa pia mafunzo ya ufundi kwa vijana kupitia chuo chake kijulikanacho kwa jina la Tarime Vocational Training College, na kwamba hadi sasa kina uwezo wa kuhudumia vijana 1,000 kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi huyo anasema PMF imeendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu na mafunzo ya ufundi kwa vijana ili kuwaandaa kuwa na mchango muhimu katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Mbali na Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime, Taasisi ya Professor Mwera pia inamiliki vyombo vya muziki kwa ajili ya kujenga na kukuza vipaji kwa wanachuo.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>HAIPPA PLC yazindua semina ya uwekezaji kwa waandishi wa habari Mara
>>Wasira kuanza ziara ya kukagua maendeleo ya CCM mkoani Mara leo
>>Mara: HAIPPA PLC yapokea wanahisa wapya zaidi ya 300, yanadi huduma zake
>>Barrick North Mara yakabidhi bilioni 3.7/- za ‘service levy’ Tarime Vijijini, bilioni 1.7/- za mrabaha kwa vijiji vitano
No comments:
Post a Comment