NEWS

Wednesday, 1 January 2025

Tumeimarisha upatikanaji wa fedha za kigeni nchini – Rais Samia



Rais Dkt Samia Suluhu Hassan akiwasilisha salamu zake za mwaka mpya 2025 kwa Watanzania kwa njia ya televisheni jana Desemba 31, 2024.
----------------------------------

Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuimarisha upatikanaji wa fedha za kigeni, hususan Dola ya Kimarekani - uliokuwa umepungua na kuathiri shughuli nyingi za biashara na uzalishaji nchini mwaka 2024.

“Tuliunda kikosi kazi cha wataalamu kilichotafiti hali hiyo [upungufu wa fedha za kigeni] na kushauri hatua za kuchukuliwa,” Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alisema jana Desemba 31, 2024 katika sehemu ya salamu zake za mwaka mpya 2025 kwa Watanzania.

Aliendelea: “Ushauri ulituongoza kutengeneza Mkakati wa Taifa wa Kuimarisha Upatikanaji wa Fedha za Kigeni. Nafarijika kwamba, kufuatia utekelezaji wa mkakati huo, upatikanaji wa fedha za kigeni umeimarika.”

Aidha, Rais Samia alisema katika kuchukua hatua za kuuhami uchumi wa nchi, serikali imefanya uamuzi wa kuweka akiba ya taifa ya dhahabu katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuongeza uhimilivu wa uchumi wa taifa.

Takwimu za BoT zinaonesha kwamba kwa kipindi cha Oktoba 2024 pekee, benki hiyo iliweza kununua kilo 872 za dhahabu safi yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 74.

Dhahabu inakubalika kama sehemu ya fedha za kigeni inapokuwa na kiwango cha usafi (purity level) kati ya asilimia 99.95 - 99.99.

Akiba ya kutosha ya fedha za kigeni inasaidia na kuendeleza imani katika kuhakikisha uimara wa thamani ya fedha ya nchi, kusaidia serikali kupata mahitaji yake ya fedha za kigeni na kulipia madeni ya nje.

Pia, akiba ya dhahabu fedha imekuwa ikitumika katika harakati za kuwezesha nchi kujikimu katika kipindi cha mtikisiko wa kiuchumi duniani, kukabiliana na majanga ya kitaifa na dharula zinazoweza kujitokeza.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages