
Mkurugenzi wa Kampuni ya Win Traders Ltd, Dkt Edward Machage akizungumza na watumishi wa Zahanati ya Surubu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime leo Januari 2, 2025.
-------------------------------
Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo na shinikizo la damu kwa wazee, pamoja na magonjwa ya watoto.
Huduma hizo zitatolewa na Daktari wa Moyo kutoka Taasisi ya Moyo - Dar es Salaam, Mtaalamu wa Vipimo kutoka Hospitali ya Rufaa Benjamin Mkapa - Dodoma na Daktari wa Watoto kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara, ambao wanaletwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Win Traders Ltd, Dkt Edward Machage kwa kushirikiana na Halmashauri hiyo.
Vituo vitakavyotumika kutolea huduma hizo ni Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime - Nyamwaga siku ya Jumamosi Januari 4 na katika Zahanati ya Surubu katani Komaswa siku ya Jumapili Januari 5, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Zahanati ya Surubu leo Alhamisi Januari 2, 2025, Dkt Machage amesema ujio wa madaktari hao ni fursa muhimu kwa wananchi wanaolazimika kusafiri kwenda kutafuta huduma hizo Musoma, Mwanza na Dar es Salaam.
Amefafanua kuwa wananchi wanaolengwa na huduma hizo ni wazee wenye umri wa miaka 50 na kuendelea, na watoto wenye umri wa 0 hadi miaka 12, na kwamba watu zaidi ya 300 wanatarajiwa kuhudumiwa.

Dkt Machage (kushoto) akiteta jambo na Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Surubu, Dkt Mokoa Samwel Roswe (katikati) na Afisa Muuguzi, Nyamizi Jumanne.
-----------------------------------
"Hii ni fursa kwa wenye matatizo ya moyo, tunaleta daktari bingwa mbobezi ambaye ataweza kufanya uchunguzi wa mioyo yao, kuwashauri vizuri na kuanza matibau yatakayofaa kwa wakati huu.
"Pia, natoa wito wazazi wenye watoto ambao wana changamoto za kiafya kukutana na daktari bingwa wa watoto kwa ajili ya huduma ya uchunguzi, ushauri na matibabu," amesisitiza Dkt Machage.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuunga juhudi za serikali katika kuboresha huduma za matibabu katika jamii. “Tumejipanga vizuri, kama watu ni wengi tutafanya kazi mchana na usiku ili kuhakikisha kuwa watakaofika kutafuta huduma hizo wanaonana na madaktari bingwa,” amesema.
Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Surubu, Dkt Mokoa Samwel Roswe amesema ujio wa huduma hizo ni fursa muhimu na ya kwanza kutokea katika eneo hilo lililopo pembezoni mwa wilaya ya Tarime.
"Wito wangu kwa ndugu zangu Watanzania wenyeji wa kijiji cha Surubu, Komaswa na kata jirani ya Manga watoke kwa mwitikio mkubwa, huduma imekuja mpaka mlangoni," amesema Dkt Roswe.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Sultani wa mwisho wa Zanzibar afariki dunia akiwa na umri wa miaka 95
>>Viongozi, wadau na waandishi wa habari wakubaliana kubeba ajenda ya maendeleo Mara
>>Simba waripotiwa kuua mifugo ya wanavijiji wilayani Serengeti
>> Mara: Wanasiasa wapigana vikumbo kujipendekeza kwa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
No comments:
Post a Comment