NEWS

Thursday, 27 February 2025

DC mpya Bunda aripoti kwa RC Mara



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi (katikati) akizungumza na Mkuu mpya wa Wilaya ya Bunda, Aswege Enock Kaminyoge (kulia) na Mkuu mpya wa Wilaya ya Maswa, Dkt Vincent Naano Anney ofisini kwake mjini Musoma leo Februari 27, 2025.
------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi amempokea Mkuu mpya wa Wilaya (DC) ya Bunda, Aswege Enock Kaminyoge aliyefika kuripoti ofisini kwake mjini Musoma leo Februari 27, 2025.

Kaminyonge alihamishwa hivi karibuni na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoka wilaya ya Maswa mkoani Simiyu. Sasa anachukua nafasi ya Dkt Vincent Naano Anney aliyehamishwa kutoka Bunda kwenda Maswa.

RC Mtambi amemtaka DC Kaminyinge kusimamia amani na utulivu, hususan mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu akisema mkoa wa Mara hautaruhusu mtu yoyote kuvuruga amani na utulivu uliopo kwa sasa.

“Shabaha yetu ni kujenga uchumi wa mkoa kwa ajili ya wananchi ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo, na hayo yatafanikiwa tu endapo amani na utulivu vitaendelea kutawala,” amesema.

Aidha, RC Mtambi amewataka wakuu wa wilaya zote za mkoa wa Mara kuwa makini na alichokiita homa za kisiasa zinazoweza kuvuruga amani na utulivu na kuutoa mkoa kwenye dhamira ya kukuza uchumi wa wananchi wake.

Vilevile, amewataka wakuu wa wilaya kuhakikisha wananchi wapo salama na wanaendelea kufanya shughuli zao kama kawaida, na wanasiasa wanafanya siasa zao kwa amani na utulivu kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya serikali.

“Pale Bunda Mji tuna madini na wananchi wapo kazini wakichimba madini yaliyogundulika katika eneo hilo na wajibu wetu kama serikali ni kuwawekea mazingira wachimbaji hao wadogo waweze kufanya shughuli zao na kulipa kodi zinazohitajika kwa serikali,” amesema.


DC Aswege Enock Kaminyoge

Kwa upande wake DC Kaminyoge amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini.

Ameahidi kutekeleza maagizo aliyompatia kwa nguvu na moyo wote na kuwaomba wananchi wa wilaya ya Bunda kumpokea na kumpatia ushirikiano.

Naye aliyekuwa DC Anney amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mtambi, kwa kufanya naye kazi vizuri kwa kipindi chote akiwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda na kuahidi kuendeleza kazi nzuri katika wilaya ya Maswa kwa maslahi mapana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages