NEWS

Friday, 28 February 2025

Trump kukutana na Zelensky leo White House kusaini makubaliano ya kuigawia Marekani madini ya Ukraine




Rais wa Marekani, Donald Trump (pichani kushoto), amesema ana "heshima kubwa" kwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky (kulia), ikiwa ni saa kadhaa kabla ya mazungumzo yao katika Ikulu ya White House.

Hayo yanakuja baada ya utawala wa Trump kushangaza washirika wake wa Magharibi kwa kufanya mazungumzo ya kwanza ya ngazi ya juu na Moscow tangu Urusi ilipoivamia Ukraine miaka zaidi ya mitatu iliyopita.

Awali, Trump alionekana kumlaumu Zelensky kwa vita hivyo na kumkosoa kwa kushindwa kuanzisha mazungumzo ya amani mapema.

"Umekuwa hapo kwa miaka mitatu," Trump alisema Jumanne iliyopita. "Ulipaswa kumaliza vita hivyo... Hukupaswa kuwa umevianzisha hata kidogo. Ungeweza kufanikisha makubaliano."

Hata hivyo, jana Alhamisi, baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, Trump aliwambia waandishi wa habari kuhusu mazungumzo yake yanayokuja na Zelensky: "Nadhani tutakuwa na mkutano mzuri sana kesho asubuhi. Tutashirikiana vizuri sana."

Alipoulizwa na mwandishi wa BBC, Chris Mason, kama bado anadhani Zelensky ni "dikteta", Trump alijibu: "Nilisema hivyo? Siwezi kuamini kama niliyasema hayo."

Zelensky anatarajia kupata aina fulani ya dhamana ya usalama kwa ajili ya Ukraine ambayo itasaidia katika makubaliano yoyote ya amani yanayoweza kufikiwa.

Alipoulizwa kuhusu dhamana hizo jana Alhamisi, Trump alisema tu kuwa yuko "tayari kwa mambo mengi", lakini anataka Urusi na Ukraine zikubaliane kwanza kabla ya kuamua hatua zitakazowekwa ili kutekeleza makubaliano hayo.

Wakati wa ziara yake leo Ijumaa, Zelensky anatarajiwa kusaini makubaliano yatakayoipa Marekani sehemu ya rasilimali adimu za madini za Ukraine.

Trump alipendekeza kuwa uwepo wa kampuni za madini za Marekani nchini Ukraine utakuwa kama kinga dhidi ya mashambulizi ya baadaye kutoka kwa Urusi.

Alipoulizwa na BBC kama angeomba msamaha kwa kumwita Zelensky "dikteta" hivi karibuni, Trump alisema haamini kama alitamka maneno hayo. Pia alimsifu Zelensky kama mtu "shujaa sana".

Trump alizungumza baada ya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, kuhusu kumaliza vita kati ya Ukraine na Russia.

Alitabiri kuwa atakuwa na "mkutano mzuri sana" na Zelensky leo Ijumaa, akisema juhudi za kufanikisha amani "zinaendelea kwa kasi kubwa."
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages