
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati) akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katani Nyanungu jana Jumatano. Kulia aliyevaa kofia ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.
-----------------------------------
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Evans Alfred Mtambi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara kufuatilia utoaji wa zabuni ya kusambaza matofali kwenye miradi ya ujenzi wa shule katika kata ya Nyanungu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
RC Mtambi alitoa agizo hilo jana Jumatano alipokwenda Shule ya Sekondari Nyanungu kukagua mradi wa maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha tano na ujenzi wa shule ya sekondari mpya katika kijiji cha Kegonga.
Kiongozi huyo wa mkoa alieleza kutoridhishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi hiyo, hivyo kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa inakamilishwa kwa wakati.
“Sasa tunakaribia mwaka mmoja tangu fedha za mradi huu mlipopokea lakini baadhi ya majengo [mabweni mawili] yapo kwenye msingi na mengine yanaendelea kukamilishwa kwa kasi ndogo, hii haikubaliki kabisa,” alisema.
Alisema kuna umuhimu wa TAKUKURU kufuatilia ili kujiridhisha na taarifa kuwa mzabuni anayesambaza matofali katika miradi hiyo amepewa zabuni katika miradi mingi ya serikali, huku akiwa hana uwezo wa kuzalisha matofali ya kutosha kwa wakati.
Pia, RC Matambi alieleza kutoridhishwa na ubora wa umaliziaji katika majengo hayo, hivyo kuwataka wasimamizi wa mradi kuwasimamia vizuri mafundi wanaoyajenga ili kazi ifanyike vizuri bila kulipua.
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyanungu, Mwalimu Casmiry Emmanuel Kanga alisema utekelezaji wa miradi hiyo umechelewa kutokana na mzabuni husika kushindwa kupeleka matofali kwa wakati kwani amepewa zabuni katika miradi mingi ya serikali.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alieleza kusikitishwa na hali ya wanafunzi wa sekondari ya Nyanungu kukosa madawati ya kukidhi mahitaji yao.
Kutokana na hali hiyo, aliitaka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuhakikisha kuwa shule zake zote zimepata madawati ya kukidhi mahitaji ya wanafunzi ifikapo Machi 30, mwaka huu.
Sambamba na agizo hilo, alitishia kusitisha malipo ya stahili za mkurugenzi na posho za madiwani wa halmashauri hiyo mpaka wanafunzi watakapopata madawati ya kuwatosheleza.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Pelagia Balozi alisema wametenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya ununuzi wa madawati katika shule zote zenye upungufu ingawa mchakato wa manunuzi bado unaendelea.
“Mgodi wa Dhahabu wa North Mara umetuhakikishia kuwa Machi 2025 wazabuni watakuwa wamepatikana na kuanza kazi ya kutengeneza madawati hayo pamoja na manunuzi mengine ya miradi ya CSR (Uwajibikaji wa Kampuni Kwa Jamii) itakayotekelezwa,” alisema Balozi.
Wakati huo huo, RC Mtambi amewataka wakuu wa wilaya mmkoani Mara kuwakamata wazazi wa wanafunzi wanaotakiwa kwenda shule ambao hawajasajiriwa mpaka sasa na hawatoi ushirikiano kwa watendaji wanaowafuatilia wanafunzi hao, ili wafikishwe mahakamani.
“Wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza ni lazima waende shule na hakikisheni hamna mzazi au mlezi wa mtoto anayeacha kumpeleka mtoto shule na kugoma kutoa ushirikiano kwa watendaji,” alisisitiza.
Katika ziara hiyo, RC Mtambi ambaye aliambatana na wataalamu kutoka ofisi yake, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, viongozi na watendaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, alizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyanungu, Shule ya Msingi Kegonga na wananchi wa kata ya Nyanungu.
No comments:
Post a Comment