
Na Mwandishi Wetu, Tarime
Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Regicheri iliyopo nje kidogo ya mji wa Tarime mkoani Mara, Paschal Thomas amefariki dunia kwa kugongwa na basi la Kisire Luxury Coach (pichani).
Ajali hiyo ilitokea jana mchana karibu na Hoteli ya Milan mjini Tarime wakati basi hilo likitokea mji wa Sirari.
Mwalimu wa malezi wa shule hiyo, Peter Chacha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba familia ya marehemu tayari imejulishwa.
"Ni kweli tukio hilo limetokea na mwanafunzi wetu wa kidato cha pili anayeitwa Paschal Thomas amefariki katika ajali hiyo, na tayari tumeijulisha familia yake kwa ajili ya taratibu zingine," Mwalimu Chacha aliiambia Mara Online News wa njia ya simu.
Mashuhuda walisema mwanafunzi huyo alikuwa na mwenzake - kila mmoja akiwa anaendesha baiskeli, ndipo wa mbele alipoingia barabarani huku wa nyuma akifanikiwa kushika breki na kusimama kabla ya kuingia barabarani.
"Walikuwa wawili (wanafunzi) na wako speed, sasa yule wa mbele ni kama breki yake ilifeli akaingia mazima barabarani, akakutana na Kisire linatoka Sirari likamgonga," alisema shuhuda huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Emmanuel Bhita ambaye ni miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya basi hilo alisema dereva alijaribu kumkwepa lakini akashindwa kutokana na mwendo mkali wa baiskeli ya mwanafunzi huyo.
"Dereva amejitahidi sana kumkwepa lakini yeye [mwanafunzi] alikuwa ameingia barabarani tayari, na baiskeli yake ilikuwa kasi akashindwa kushika breki, ni huzuni kwa kweli," alisema Bhita.
Kamanda wa Mkoa wa Polisi Tarime Rorya hakupatikana haraka kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Kata za Mwema, Susuni, Bumera zafikiwa na msaada wa vitabu vya sekondari kutoka Nyambari Nyangwine Foundation
>>Tarime: Heche kuchinja ng’ombe 20 kujipongeza kwa ushindi CHADEMA
>>Sekondari ya Nyamongo na nyingine 4 zapokea msaada wa vitabu kutoka Taasisi ya Nyambari Nyangwine
>>Hali za MNEC Gachuma, DC Kemirembe zaimarika, waruhusiwa hospitalini Bugando
No comments:
Post a Comment