
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka akihutubia mkutano wa wastaafu mjini Musoma juzi.
--------------------------------
Serikali imeitaka mifuko ya hifadhi ya jamii na taasisi mbalimbali mkoani Mara kuheshimu utu wa wastaafu kwa kuwatendea haki, kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili.
Hayo yamo kwenye hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi - iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka alipomwakilisha katika mkutano wa wastaafu uliofanyika mjini Musoma juzi.
Alisema uhakiki wa wastaafu unaofanyika kila mwaka unatweza utu wao kutokana na kusafiri mwendo mrefu kwenda kuhakikiwa, huku wengi wao wakiwa na matatizo ya kiafya na kifedha.

Chikoka alisema atahakikisha kero za wastaafu zinashughulikiwa na vyombo vinavyohusika. Kero hizo ni pamoja na kucheleweshewa stahiki zao za uhamisho wakati walipokuwa kazini na kutopata nyongeza ya pensheni ya kila mwaka tangu mwaka 2015 hadi leo, kwa mujibu wa GN No 285 ya 2015.
Aidha, aliahidi pamoja na mambo mengine, kuwashirikisha wastaafu katika mamlaka mbalimbali za maamuzi, ikiwa ni pamoja na vikao vya Kamati za Ushauri za Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC).

Mkutano huo ulioitishwa na Umoja wa Wastaafu Tanzania (REAT) ulikukwa na madhumuni ya kusajili wanachama wake wapya, una malengo ya kutetea na kulinda haki na maslahi bora kwa wastaafu.
Madhumuni mengine ya REAT ni pamoja na kuwa jukwaa la kupaza sauti za wastafuu, kuchambua changamoto zinazowakabili wastaafu, kuwa chombo ambacho kitakuwa daraja la kuwezesha ushirikiano na serikali, vyama vya wafanyakazi, mifuko ya hifadhi ya jamii na mabenki.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii kama vile PSSSSF, NSSF na HAZINA, NHIF, NMB, TCB na wastaafu zaidi ya 500.
No comments:
Post a Comment