
Nyumbu na pundamilia katika Hifadhi ya Taifa Serengeti
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeshauriwa kujipanga kuepusha ajali za wanyamapori kugongwa na magari katika barabara ya Musoma-Mwanza eneo la Nyatwali, magharibi mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Hivi karibuni, eneo la Nyatwali linalofahamika kama Ghuba ya Speke lenye ukubwa wa ekari 14,250 katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara lilichukuliwa na serikali kuwa sehemu ya hifadhi hiyo.
Taarifa zinasema kwa sasa makundi ya wananyamapori wanaovuka barabara huko Nyatwali yameongezeka baada ya eneo hilo kuunganishwa na Hifadhi ya Taifa Setengeti.
Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA waliofanya ziara huko Jumanne iliyopita, walisema ni muhimu kuwa na mpango wa kuhakikisha wanyamapori wanatembea kwa uhuru bila ajali za kugongwa na magari katika eneo hilo.
Katika ziara hiyo, wajumbe hao walikagua maendeleo ya uhamaji wa hiari wa waliokuwa wanaishi kata ya Nyatwali iliyokuwa inaundwa na mitaa ya Tamau, Kariakoo, Nyatwali na Serengeti.
Baada ya kupata taarifa kutoka kwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Stephano Msumi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, wajumbe hao wakiongozwa na CPA Hadija Ramadhani, walijionea majengo yaliyobomolewa, na asilimia kubwa ya wananchi wakiwa wameshahama, huku ulipaji fidia ya makaburi ukiendelea.
“Mmefanya kazi nzuri, tumeona ushirikiano wa wizara, TANAPA, wilaya hadi mkoa, sasa mjitahidi kufuatilia fedha zilizobaki ili kukamilisha zoezi hili, na kama mlivyosema kwenye taarifa wanyama ni wengi wanavuka kwenda Ziwa Victoria, hivyo mjipange namna ya kupunguza wanyama kugongwa,” Dkt Robert Fyumagwa.
Akizungumza ofisini kwake, baada ya kupokea ugeni huo, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt Vincent Naano Anney aliomba utangazaji wa eneo la Nyatwali kama sehemu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti uhusishe Ziwa Victoria.
“Ziwa Victoria litangazwe kama bidhaa inayounganisha Hifadhi ya Taifa Serengeti. Hoteli zijengwe eneo hilo ili watalii waweze kufika upande huu kwa maana wanyama watakuwa wengi na itakuwa fursa ya kiuchumi kwa wananchi wa Bunda na mkoa wa Mara kwa ujumla,” alisema.
Kuhusu ukamilishaji wa malipo ya fidia za makaburi, Dkt Naano alisema: “Tunatarajia mpaka tarehe ishirini mwezi huu [Februari] ulipaji fidia ya kuhamisha makaburi liwe limekamilika, wabaki wale wachache ambao fedha zao zitakuja, ili kuepuka migongano.”
No comments:
Post a Comment