
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Daniel Komote akizungumza katika kikao cha madiwani jana Februari 4, 2025.
-------------------------------
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji wa Tarime, mkoani Mara limepitisha bajeti ya shilingi bilioni 30.851 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali
Hatua hiyo ilifikiwa katika kikao cha kawaida cha robo ya pili (Oktoba hadi Desemba 2024) kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo jana Februari 4, 2025.
Asilimia 40 ya kiasi hicho cha fedha kitatumika kugharimia shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi, na asilimia 60 ni kwa ajili ya shughuli za ofisi na mishahara kwa watumishi.

Madiwani kikaoni. (Picha zote na Mara Online News)
----------------------------------
Pamoja na mambo mengine, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Daniel Komote aliwapongeza wafanyabiashara kwa kulipa kodi kwa uaminifu bila shuruti hali ambayo alisema inawezesha miradi ya maendeleo kutekelezeka kwa urahisi kupitia mapato na ya ndani.
“Wapelekeeni salamu wafanyabiashara wa Tarime kwa namna wanavyolipa kod,i hakuna mfanyabiashara aliyewahi kufikishwa mahakamani kwamba amegoma kulipa kodi,” alisema Komote ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nkende kwa tiketi ya chama tawala - CCM.
Aidha, kwa mjibu wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Afya na Elimu, baraza hilo limethibitisha uwepo wa dawa za kutosha kwenye zahanati zote ndani ya halmashauri hiyo.
“Tumetembelea vituo vyote tunazo dawa za kutosha katika vituo vyote,” alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Daudi wangwe ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kitare (CCM).
Hivyo, wananchi wameombwa kwenda kupata huduma kwenye zahanati zilizo jirani na maeneo yao ili kuepuka usumbufu wa kwenda kutafuta huduma kwenye Hospitali ya Wilaya.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele alimwagiza Afisa Mazingira wa Halmashauri hiyo kuhakikisha uchafu unaorundikwa jirani na Hospital ya Wilaya unaondolewa ili kuepusha magonjwa ya mlipuko.
“Nilishatoa maelekezo eneo lile la Hospitali nisione uchafu. Afisa Mazingira na mtu wa usafi nisisikie tena uchafu kuwepo katika eneo lile, fanya utaratibu uchafu ule utoke,” alisisitiza DC Gowele.
No comments:
Post a Comment