
Prof Philemon Mikol Sarungi enzi za uhai
Na Mwandishi Wetu, Dar
Mamia ya waombolezaji leo Machi 10, 2025 wamekusanyika katika ukumbi maarufu wa Karimjee jijini Dar es Salaam kuaga mwili wa waziri wa zamani na daktari bingwa wa mifupa, Prof Philemon Mikol Sarungi, aliyefariki dunia Machi 5, 2025.
Waombolezaji hao wameongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, ambaye amemwakilisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa waombolezaji hao walikuwepo viongozi mashuhuri, wakiwemo Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Jaji Joseph Sinde Warioba, Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana, Mkurugenzi wa Taaisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kwa kutaja wachache.
Akitoa salaamu zake kwa niaba ya Rais Samia, Waziri Kikwete amemweleza hayati Prof Sarungi kwamba alikuwa mtu asiyekuwa na mipaka ya upendo kwa watu, mtaalamu bingwa na mnyenyekevu.
Jaji Joseph Warioba ambaye alipata fursa ya kufanya kazi serikalini na Prof Sarungi, amesema alikuwa mwalimu, mtaalamu na kiongozi aliyejaliwa tunu ya kutokuwa na mbwembwe.
Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amewambia waombolezaji kuwa Prof Sarungi hakuwa mtu mnafiki na alificha mapenzi yake kwa Klabu ya Simba, na kwamba angekuwepo angekemea vitendo vya upuuzi vinavyoingizwa kwenye sekta ya mpira wa miguu nchini.
Zitto amependekeza Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili ipewe jina la Profesa Philemon Sarungi kutokana na juhudi zake kubwa za kuboresha sekta ya afya, hasa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Prof Sarungi (Machi 23, 1936 – Machi 5, 2025) aliitumika serikali katika nyadhifa mbalimbali akianzia kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Muhimbili na waziri wa wizara mbalimbali.
Alipendwa na watu wengi kutokana na tabia yake ya ucheshi na kujichanganya na watu wa tabaka zote katika jamii bila kujali cheo chake.
Wananchi wengi walizidi kumpenda pale alipokuwa akivua suti zake za uwaziri, au ukuu wa mkoa na kuvaa majoho ya udaktari, hasa wakati wa kuhudumia wahanga wa ajali.
No comments:
Post a Comment