
Rais na CEO wa Barrick, Dkt Mark Bristow (katikati waliokaa), Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (wa tatu waliokaa), Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Petro Kurate (wa pili waliokaa), viongozi wa kata na vijiji, na wafanyakazi wa mgodi wa North Mara wakifurahia picha ya pamoja mara baada ya makabidhiano ya hundi za malipo ya mrabaha na ushuru wa huduma Januari 24, 2025.
--------------------------------------
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, moja ya migodi mikubwa nchini Tanzania, unaendelea kushuhudia matokeo chanya kwa uwekezaji na maendeleo endelevu kwa mgodi huo na jamii inayouzunguka tangu ulipokabidhiwa kwa kampuni ya Barrick mwaka 2019 hadi sasa.
Kwa kufanya kazi kwa karibu na serikali na jamii, Barrick katika mgodi huo imefanikisha mabadiliko makubwa ya kimaendeleo, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kijamii, utoaji ajira na zabuni kwa wazawa, urejeshaji gawio la mrabaha kwa vijiji vitano, kuimarisha usimamizi wa mazingira, kuhuisha maisha ya mgodi na kupunguza vitendo vya uvamizi mgodini.
“Kuna mabadiliko makubwa yametokea katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara tangu 2019 hadi sasa,” Meneja Mkuu (GM) wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko aliiambia Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti ilipofanya ziara mgodini hapo, hivi karibuni.
GM Lyambiko alisema wakati Barrick inachukua dhamana ya kuendesha mgodi huo ilikuta unakabiliwa na changamoto kubwa ya kimazingira, miongoni mambo mengine, lakini yote kwa sasa yamebaki historia.
CSR na miradi ya kijamii
Barrick kupitia mpango wake wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR), imeendelea kutoa mabilioni ya shilingi kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kijamii katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa Morth Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa ujumla.
Taarifa zinaoseha hadi sasa mgodi huo umetumia takribani dola za Marekani zaidi ya milioni 15 kwenye miradi ya kijamii na hivyo kuwa moja ya wadau wakubwa wanaunga juhudi za serikali katika kuboresha maisha ya wananchi katka wilaya hiyo.
Mfano, mwaka 2024 mgodi huo ulitenga shilingi bilioni tisa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii ipatayo 101.
Miradi inayolengwa na fedha hizo za CSR ni elimu, afya, maji, barabara na kilimo - ambayo ina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi.
“Miradi hii inasaidia pia kukuza na kudumisha mahusiano yetu na jamii,” anasema GM Lyambiko.
Mbali na CSR, mgodi wa North Mara unalipa kodi mbalimbali, zikiwemo ushuru wa huduma (service levy) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. Mfano, Januari 24, mwaka huu uliipatia shilingi bilioni 3.709, ikiwa ni malipo ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Mrabaha kwa vijiji vitano
Mara baada Barrick kukabidhiwa mgodi wa North Mara mwaka 2019, ilianza kutafuta namna ya kurejesha malipo ya gawio la mrabaha kwa vijiji vitano vya Nyangoto, Kerende, Nyamwaga, Genkuru na Kewanja ambavyo ni miongoni mwa vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi huo.
Vijiji hivyo vitano ni ambavyo vilikuwa na haki ya kuchimba dhahabu kwenye shimo la Nyabigena (ambalo ni sehemu ya mgodi wa North Mara) kabla ya Barrick kukabidhiwa uendeshaji wa mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals kuanzia mwaka 2019.
Hivyo, Barrick ilifanya tafiti za kijiolojia katika shimo la Nyabigena na kufanikiwa kuanza tena uzalishaji wa dhahabu katika robo ya pili ya mwaka 2023, baada ya kuwa umesimama tangu mwaka 2017.
Kurejea kwa uzalishaji katika shimo hilo kumevipatia vijiji hivyo matumaini mapya ya kuendelea kupata gawio la mrabaha kama ilivyokuwa awali. Malipo ya mrabaha hufanyika kila robo ya mwaka kutokana na hali ya uzalishaji na uuzaji wa dhahabu.
Mfano, Desemba 9, 2024, vijiji hivyo vilipata gawio la mrabaha la shilingi bilioni 2.1, ikiwa ni malipo ya robo ya tatu ya mwaka 2024, na Januari 24, mwaka huu mgodi huo ulivipatia vijiji hivyo gawio la mrabaha la shilingi bilioni 1.718 ambazo ni malipo ya robo ya nne ya mwaka jana.
Kwa mujibu wa GM Lyambiko, malipo hayo yanafanya gawio la mirabaha lililotolewa na mgodi wa North Mara kwenda katika vijiji hivyo kutokana na uzalishaji wa Aprili 2023 hadi Septemba 2024 kufikia shilingi bilioni 5.1.
Hiyo ni sehemu ya juhudi za Barrick za kuhakikisha kwamba faida ya rasilimali ya dhahabu inayochimbwa katika mgodi wa North Mara inarejeshwa kwa jamii inayouzunguka na kuhakikisha inapata huduma bora za kijamii.
Ajira, zabuni kwa wazawa
Mgodi wa North Mara umeendelea kuongeza ajira kwa wazawa tangu Barrick ichukue dhamana ya kuuendesha. Hadi sasa asilimia 96 ya wafanyakazi wa mgodi huo ni Watanzania, kwa mujibu wa GM Lyambiko.
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti iliongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Josephat Kandege, ilipofanya ziara katika mgodi wa North Mara iliupongeza kwa jinsi unavyojizatiti kushirikiana na kuboresha uhusiano na jamii inayouzunguka.
Pamoja na kuajiri wafanyakazi wazawa, taarifa zinasema mgodi wa North Mara umeendelea kuongeza idadi ya wazabuni wazawa wanaosambaza bidhaa na utoaji wa huduma mbalimbali mgodini.
Hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa faida ya mgodi wa North Mara haikai kwa kampuni tu, bali inatiririka pia kwa wafanyabiashara wazawa na kuinua uchumi wa jamii inayouzunguka.
Usimamizi wa mazingira
Kwa upande wa mazingira, mgodi wa North Mara umekuwa ukifanya juhudi za kisayansi na kiteknolojia za kupunguza athari za uchimbaji wa madini kwa mazingira.
Uwekezaji mkubwa umefanyika kwa teknolojia za kisasa za uchimbaji na usindikaji wa madini ili kupunguza matumizi ya kemikali hatari na kuimarisha usimamizi wa maji na ardhi.
“Kulikuwa na chanagmaoto kubwa ya kimazingira lakini uwekezaji mkubwa umefanyika,” anasema GM Lyambiko.
Hatua hizo zinasaidia kuepusha madhara kwa mazingira na kuhakikisha kuwa uchimbaji wa madini katika mgodi huo unafanywa kwa njia endelevu isiyo na athari kwa jamii na mazingira.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti, Josephat Kandege (wa pili kutoka kulia mbele), Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko (kulia mbele), wajumbe wa kamati hiyo na viongozi mbalimbali wakitembelea mgodi huo wilayani Tarime hivi karibuni.
-------------------------------------
Maisha ya mgodi
Mageuzi mengine yaliyofanyika ni kuongeza maisha mgodi wa North Mara, na hivyo kuleta matumaini ya kuendelea kwa ajira na maendeleo ya kiuchumi kwa jamii inayozunguka mgodi huo.
“Kuna mabadiliko makubwa yametokea na maisha ya mgodi sasa yatakuwa hadi mwaka 2040 badada ya mwaka 2028,” anasema GM Lyambiko.
Hatua hiyo pia inathibitisha dhamira ya kampuni ya Barrick katika kuhakikisha usimamizi bora wa rasilimali na kuendelea kuchangia maendeleo ya taifa.
Kupungua kwa uvamizi
Pia, yameshuhudiwa mafanikio ya kupunguza kwa vitendo vya kuvamia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara vinavyofanywa na makundi ya watu wanaofahamika zaidi kwa jina la intruders.
Mafanikio hayo yanatokana na juhudi za pamoja za mgodi, serikali na jamii katika kuweka mikakati ya kuhakikisha usalama na kudhibiti uvamizi mgodini.
Kwa kushirikiana na serikali na viongozi wa kijamii wakiwemo wazee wa mila, mgodi huo umeweza kupunguza migogoro na kuhakikisha kuwa rasilimali zinatumiwa kwa manufaa ya wote.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi Shule ya Msingi mpya ya kisasa ya Kenyangi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mwishoni mwa mwaka jana, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Barrick, Dkt Mark Bristow, alieleza kuridhishwa na juhudi za pamoja zinazofanywa katika kukabiliana na tatizo hilo.
“Tumepata mafanikio makubwa sana katika kukabiliana na wavamizi. Kwa mfano, idadi ya wavamizi ilipungua kutoka 381 Aprili hadi 65 Agosti [mwaka 2024], hivyo tupo kwenye njia sahihi,” alisema Dkt Mark.
“Napenda kuwapongeza watu mbalimbali akiwemo mbunge, madiwani, wajumbe wa CDC, wenyeviti wa vijiji na wazee wa mila kwa kazi kubwa mliyofanya kuhakikisha vijana wanaovamia mgodi wanaacha uhalifu huo.
“Sisi ni jamii moja, na mnaona hata leo tunafurahia matunda ya ushirikiano na ujirani mwema. Tuendelee kushirikiana ili tuendelee kuvuna matunda ya mgodi huu,” alisisitiza Dkt Mark.
Kamati ya Bunge yafurahishwa
Machi 7, 2025, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti ilifanya ziara katika mgodi wa North Mara na kueleza kufurahishwa na taarifa ya shughuli na maendeleo ya mgodi huo iliyotolewa na GM Lyambiko, kabla ya kutembelea kinu cha kuchenjua dhahabu.
“Tumepata fursa ya kujua mgodi unavyofanya kazi na unavyoshirikiana na jamii kutatua changamoto nyingi. Mfano uboreshaji wa huduma ya maji katika vijiji vinne tayari vinapata maji safi ya kunywa,” alisema Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Josephat Kandege.
Kandege ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kalambo mkoani Rukwa, alieleza kufurahishwa na uwepo wa wafanyakazi wengi Watanzania katika mgodi huo, akiwemo Meneja Mkuu.
Wajumbe wa kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti pia wamepongeza kampuni ya Barrick kwa kuendelea kuzingatia sheria za nchi, ikiwemo za kodi na hivyo kuwa na mchango mkubwa kwa mapato ya taifa.
Wabunge hao pia wameonesha kufurahishwa na kiasi kikibwa cha fedha kinachotolewa na kampuni ya Barick kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia mpango wake wa CSR.
“Takwimu zinaonesha Barrick North Mara inatumia sio chini ya shilingi bilioni saba kwenye miradi ya CSR kila mwaka, kwa kweli ni pesa nyingi na inagusa sana jamii,” alisema Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Mathayo ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo.
Naye Mbunge wa Viti Maalum ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, Stella Ikupa Alex aliipongeza Barrick kwa kuendelea kufanya vizuri kisekta, huku akitolea mfano wa tuzo mbalimbali ambazo imetunukiwa, ikiwemo ya mwajiri bora nchini. “Tuzo hizi ni nyingi, nami niwapongeze Barrick na CSR yenu inaonekana kwa ukubwa sana,” alisema.
Pia, Mbunge wa Jimbo la Meatu, Leah Komanya, aliupongeza mgodi huo kwa kutumia takriban shilingi bilioni moja kujenga Kituo cha Afya Genkuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. “Ujenzi wa Kituo cha Afya Genkuru ambao umefanywa na mgodi ni jambo zuri sana, niwapongeze pia kwa kutunza mazingira na kutengeneza ajira kwa vijana,” alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ole, Juma Hamad Omar aliipongeza Barrick kwa kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu katika mpango wake wa CSR, huku pia akieleza kuridhishwa na uwasilishaji uliofanywa na GM Lyambiko mbele ya kamati hiyo.
Awali, GM Lyambiko, amesema mgodi huo umetumia zaidi ya dola za Kimarekani milioni 15 kwenye miradi ya maendeleo ya jamii kupitia CSR.
Siri ya mafanikio
Mageuzi makubwa ya maendeleo yaliyowezeshwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara tangu 2019, ni matokeo ya ushirikiano kati ya mgodi huo chini ya kampuni ya Barrick, serikali na jamii inayouzunguka.
Kwa kupitia mipango bora ya CSR ya Barrick North Mara, maendeleo ya kijamii na utunzaji wa mazingira, uchimbaji wa madini unaweza kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Ni wazi kuwa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara chini Barrick, utaendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo yanayouzunguka na kuinua uchumi wa taifa.
No comments:
Post a Comment