
Walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Manga wakipokea msaada wa photocopy machine kutoka kwa Eliakim Maswi aliyewakilishwa na John Waigama kama mgeni rasmi katika Mahafali ya Tisa ya Kidato cha Sita shuleni hapo Machi 13, 2025.
-----------------------------------
Shule ya Sekondari Manga iliyopo kata ya Komaswa wilayani Tarime, Mara imepokea msaada wa photocopy machine, kompyuta mbili, pamoja na laptop ya kisasa kwa ajili ya Mkuu wa Shule.
Msaada huo ulitolewa na mgeni rasmi katika Mahafali ya Tisa ya Kidato cha Sita ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo jana Machi 13, 2025.
Mgeni rasmi alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, ambaye aliwakilishwa na John Waigama.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Manga, Mwalimu Editha Lazaro Nakei Alimshukuru Maswi kwa kuipatia shule hiyo vitendea kazi hivyo akisema vitachochea kuimarika kwa taaluma shuleni hapo.

Mkuu wa Shule, Mwalimu Nakei (kushoto mbele), akimuongoza mgeni rasmi alipowasili shuleni hapo.
---------------------------------

Mkuu wa Shule ya Sekondari Manga, Mwalimu Editha Lazaro Nakei na wahitimu wa kidato cha sita wakiimba na kucheza kwa madaha wakati wa mahafali hayo.
------------------------------------
Kwa upande mwingine, Mwalimu Nakei na wahitimu hao wa kidato cha sita waliahidi matokeo bora zaidi katika Mtihani wa Taifa ujao.
"Wanafunzi hawa matazamio na matarajio yao mwaka huu ni kuishia daraja la pili. Elimu tuliyowapa itawasaidia na kuwa msingi mzuri wa kujiunga na vyuo vikuu na vyuo vya kati, kutunza mazingira, uwezo mzuri wa kujitambua, kufikiri na kufanya maamuzi sahihi katika kazi zao za ujenzi wa taifa letu.
"Pia, elimu tuliyowapatia itawawezesha kuwa na ari ya kudadisi na kufanya kazi kwa bidii bila kusukumwa ili kuendana na kaulimbiu ya Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan - ya Kazi Iendelee,” alisema Mwalimu Nakei.
Mwalimu Nakei alisema wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita ni 411 kati ya 486 wote wa kike walionza masomo shuleni hapo mwaka 2023, na kwamba idadi hiyo ilipungua kutokana na sababu za ugumu wa maisha, vifo na magonjwa.

Waigama (wa pili kushoto) akimwakilisha Maswi kukabidhi msaada wa kompyuta kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Manga, Mwalimu Editha Lazaro Nakei.
--------------------------------------

Waigama (wa pili kushoto) akimwakilisha Maswi kukabidhi msaada wa laptop kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Manga, Mwalimu Editha Lazaro Nakei.
---------------------------------------

Mgeni rasmi akikabidhi vyeti kwa wahitimu
"Mnapoelekea hatua inayofuata elimu ya chuo kikuu, mafunzo ya ufundi au kujiunga na sekta ya ajira, kumbukeni kuwa hakuna mafanikio yanayokuja kwa bahati nasibu, bali kwa juhudi na nidhamu. Dunia ya leo ina ushindani mkubwa, hivyo ni muhimu kuwa na maono, bidii na kujituma,” alisema Waigama na kuendelea:
"Msiogope changamoto, badala yake ziwe chachu ya mafanikio. Taifa linahitaji vijana wenye maono na walio tayari kuchangia maendeleo ya nchi. Elimu ni nguzo ya maendeleo ya taifa na mwalimu ndio msingi wa kujenga kizazi chenye maarifa na maadili. Tunawaombea mfanye vema, kumbukeni mafaniko ni matokeo ya juhudi na uvumilivu."

Wazazi wakichangia fedha za kununua tenki la maji shuleni, ambapo shilingi milioni tatu zilipatikana. Kati ya hizo, Maswi na Waigama kila mmoja alitoa shilingi milioni moja, huku milioni moja nyingine ikichangwa na wazazi na wadau mbalimbali.
------------------------------------

Mgeni rasmi akikabidhi cheti kwa mhitimu

Mmoja wa wahitimu akionesha ubunifu wa vazi na urembo.
No comments:
Post a Comment