NEWS

Saturday, 29 March 2025

Mgodi wa Barrick North Mara waanza kukabidhi madawati ya CSR Tarime Vijijini, DC Gowele ataka kasi ya utengenezaji



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (katikati mbele), mwakilishi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Mwita Magige (wa nne kushoto), Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi (wa tatu kushoto) na viongozi wengine wakifurahia makabidhiano ya madawati katika Shule ya Msingi Kewanja leo Machi 29, 2025.
---------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara umeanza kukabidhi sehemu ya madawati zaidi ya 9,000 yanayotarajiwa kutengenezwa kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), mkoani Mara.

Madawati hayo yanatengenezwa kwa gharama ya shilingi milioni 898 za mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) wa kampuni ya Barrick inayoendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Akizungumza katika hafla ya kupokea na kukabidhi madawati 215 kwa Shule ya Msingi Kewanja leo Machi 29, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, ameushukuru mgodi huo kwa kutoa fedha za CSR kugharamia utengenezaji wa kile alichokiita idadi kubwa ya madawati, viti na meza ili kukabili upungufu wa madawati ya wanafunzi.

Sehemu ya madawari yaliyokabidhiwa 
katika Shule ya Msingi Kewanja.
-------------------------------------

Meja Gowele amesema shule za msingi na sekondari katika halmashauri hiyo zinakabiliwa na upungufu wa madawati kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi baada ya wazazi na walezi kuitikia wito wa serikali wa kupeleka watoto shule.

“Tunatarajia idadi kubwa ya madawati ili kutatua changamoto iliyopo. Tunaushukuru mgodi kwa kuitikia na kutekeleza mradi huu,” amesema Meja Gowele.

Meja Gowele ambaye amefuatana na viongozi mbalimbali, wakiwemo madiwani na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Solomon Shati, ameutaka mgodi huo kuongeza kasi ya utengenezaji wa mdawati yanayohitajika, huku akisema Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, anatarajiwa kupokea na kukabidhi sehemu nyingine ya madawati siku chache zijazo.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza katika hafla hiyo ya kukabidhi madawati.
----------------------------------------

Meja Gowele ametumia fursa hiyo pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji, jambo ambalo lina faida kwa taifa - akitolea mfano wa uwekezaji mkubwa kwenye maendeleo ya jamii unaofanywa na kampuni ya Barrick katika halmashauri hiyo.

Kwa mujibu wa Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi, mgodi huo umeelekeza tenda za kutengeneza madawati hayo kwa wakandarasi wazawa.

“Mradi huu wa kutengeneza madawati ni miongoni mwa miradi 101 ya kijamii itakayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mwaka huu kutokana na shilingi bilioni tisa za CSR Barrick North Mara,” amesema Uhadi.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mwita Magige, amesema utengenezaji wa madawati hayo zaidi ya 9,000 ni utekelezaji wa azimio la madiwani wa halmashauri hiyo.


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (aliyevaa kofia nyeusi), akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi, wakati wa kupokea na kukabidhi madawati katikati Shule ya Msingi Kewanja.                                        
  ---------------------------------------------------
 
“Madawati yanayotengenezwa yatagawanywa kulingana na mahitaji ya shule husika, hivyo tunaamini sasa hakuna mwanafunzi ambaye atakaa chini, maana hata halmashauri imetenga shilingi milioni 300 za mapato ya ndani kwa ajili ya kutengeneza madawati” amesema Magige ambaye ni Diwani wa Kata ya Nyamwaga.

Naye Kaimu Afisa Elimu Shule za Msingi wa halmashauri hiyo, Mwalimu Marina Ngailo, amesema madawari hayo yatasaidia kuinua taaluma na kupunguza utoro wa wanafunzi. shuleni.

“Tunaushukuru mgodi na serikali kwa hatua hii ya kutengeneza madawati, tunaamini yatasaidia kuongeza ufaulu wa mitihani katika shule zetu, pamoja na kupunguza utoro wa wanafunzi shuleni, kwani adha ya kukaa chini itakuwa imeisha,” amesema Mwalimu Ngailo.

Mradi huo wa kutengeneza madawati zaidi ya 9,000 kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara umekuja wakati mwafaka, kwani halmashauri hiyo inaripotiwa kukabiliwa na upungufu mkubwa wa samani hizo kutokana na ongezekeo kubwa la wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages