
Dkt Wison Mukama (aliyevaa suruali ya bluu), akizungumza na wanamichezo wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Klabu Bingwa 2025 yaliyofanyika wilayani Bunda, mkoani Mara.
------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Bunda
Mdau wa maendeleo, Dkt Wison Mukama, ametajwa kuwa na mchango mkubwa kuwahi kutokea katika historia ya maendeleo ya michezo ya mpira wa mikono Tanzania.
Hayo yalielezwa hivi karibuni kwenye ufunguzi wa Mashindano ya Klabu Bingwa ya Mpira wa Mikono nchini, yaliyofanyika katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara - ambapo mgeni rasmi alikuwa Dkt Mukama.
“Dkt Mukama ana mchango mkubwa kwenye michezo hii, na kwenye mashindano haya ametoa shilingi milioni 6.5 kusaidia kuyafanikisha,” Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Mikono Tanzania (TAHA), Yehoshefati Kalulu alisema.
Kalulu aliongeza: “Siyo hivyo tu, Mr Mukama amesaidia vitu vingi - tunamshukuru sasa, na anaweza akasaidia hata upande wa zawadi. Sisi katika historia yetu ya TAHA yawezekana hatujawahi kumpata mtu ambaye ametu- support kama Mr Mukama.”

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu huyo wa TAHA, Kalulu, historia ya maendeleo ya michezo ya mpira wa mikono Tanzania haiwezi kukamilika bila kutaja jina la Dkt Wilson Mukama na mchango wake.
“Tumetengeneza historia na Mr Mukama kwa sababu amewiwa kusaidia chama chetu, hivyo tutaendelea kumtumia, naye ameahidi kuendelea kutupa ushirikiano - kama kuna changamoto yoyote basi tuwasiliane ili aweze kutusaidia,” Kalulu alisema.
Kalulu alitumia nafasi hiyo pia kuomba wadau wengine kujitokeza kuchangia maendeleo ya TAHA, kuhu akidokeza shauku yake ya kuona mkoa wa Mara unakuwa na miundombinu rafiki ya michezo ya mpira wa mikono.
“Tunatamani sana hata kwa mkoa wa Mara tuweze kuwa na uwanja wa kisasa ili kupata fursa za kuwa wenyeji wa mashindano makubwa,” alisema na kubainisha kuwa mashindano hayo yalishirikisha vilabu vya mpira wa mikono kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Hiyo ni mara ya tatu kwa mashindano hayo kufanyika Bunda. Mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2022, kisha mwaka 2023 na sasa mwaka 2025.
“Mashindano haya yanafanyika Bunda kwa sababu Bunda na mkoa wa Mara kwa ujumla mpira wa mikono unachezwa sana, unapendwa sana, lakini pia una mashabiki wengi, hasa Bunda imekuwa ikifanya vizuri kwenye michezo hii huku Kanda ya Ziwa,” alisema Kalulu.
Aidha, kiongozi huyo wa TAHA alisema mpira wa mikono umekuwa na manufaa kwa vijana wengi kutoka Bunda na maeneo mengine ya mkoa wa Mara, kwani kupitia michezo hiyo baadhi yao wameweza kupata ajira kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, likiwemo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
No comments:
Post a Comment