
Kushoto ni muonekano wa Kanisa la AGGCI Nyamwaga - Tarime Vijijini, ambalo jana Jumapili liliendesha harambee ya kuchangia ukarabati wake, ambapo Nyambari Nyangwine (pichani kulia) alilichangia shilingi milioni tatu.
------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Tarime
Aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime kwa tiketi ya chama tawala - CCM, Nyambari Nyangwine, ameendelea ‘kupiga tafu’ madhehebu ya dini, ambapo jana Jumapili alichangia shilingi milioni sita katika makanisa mawili tofauti katika wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Makanisa hayo ambayo kila mmoja limepata mchango wa shilingi milioni tatu kutoka kwa Nyambari, ni Kanisa Katoliki Kigango cha Mtana, Parokia ya Komaswa na Kanisa la Assemblies of God Gospel Church International (AGGCI) Nyamwaga.
Makanisa hayo kila moja lilifanya harambee katika ibada ya jana Jumapili, huku Nyambari ambaye ni mfanyabishara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini akiwakilishwa na wasaidizi wake.
Katika harambee ya Kanisa Katoliki Kigango cha Mtana, Parokia ya Komaswa ya kuchangia ununuzi wa kinanda cha kwaya ya kanisa hilo, zilipatikana shilingi milioni 5.492, ambapo Nyambari kupitia mwakilishi wake, Ambrose Chacha Nyangoko alichangia shilingi milioni tatu.
Mwakilishi wa Nyambari Nyangwine, Ambrose Chacha Nyangoko, akizungumza wakati wa harambee hiyo.
--------------------------------------
Kwa upande wake, Paroko wa Kanisa hilo, Padre Joseph Nyamaho Nyagechanga, alimshukuru Nyambari akisema: "Anayekujali wakati wa shida ndiye ndugu yako na rafiki wa kweli, tumuombee na kumshukuru Nyambari Nyangwine, ameonesha nia kuu katika kusaidia maendeleo ndani ya kanisa."
Padre Nyamaho aliongeza: "Mfikishie Nyambari Nyangwine salamu, tumeshukuru sana - sana kwa mchango huu alioutoa kwa ajili ya maendeleo na ukuaji na uinjilishaji ndani ya kanisa.”
Viongozi, waumini na wageni waalikwa wa Kanisa Katoliki Kigango cha Mtana, Parokia ya Komaswa wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ibada na harambee hiyo.
------------------------------------
Kwa upande wa harambee ya kuchangia ukarabati wa Kanisa la AGGCI Nyamwaga, zilipatikana shilingi milioni 6.24, zikiwemo milioni tatu zilizotolewa na Nyambari kupitia mwakilishi wake, Keberera Chacha.
Mchungaji wa Kanisa la AGGCI Nyamwaga, Kennedy Rwaya Chacha, akizungumza wakati wa harambee hiyo.
-------------------------------------
Naye Katibu wa kanisa hilo, Emmanuel Chibuga alisema: "Tunashukuru sana kwa tukio la leo la harambee katika kanisa letu na tumeutambua mchango wa Nyambari Nyangwine wa shilingi milioni tatu, Mungu ambariki na azidi kutoa ushirikiano panapohitajika."
Mapema mwezi huu wa Machi 2025, Nyambari alishiriki katika harambee mbili kama mgeni rasmi na kuchagisha shilingi zaidi ya milioni 45 katika makanisa ya SDA Nyabitocho na KMT Mangucha.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
»Askari Magereza wawili mbaroni mwa Polisi kwa mauaji ya mwanakijiji wilayani Serengeti
»Dkt Mukama aweka alama Chama cha Mpira wa Mikono, apiga jeki mashindano ya Klabu Bingwa yaliyofanyika Bunda
»Mgodi wa Barrick North Mara waanza kukabidhi madawati ya CRS Tarime Vijijini, DC Gowele ataka kasi ya utengenezaji
No comments:
Post a Comment