
Taswira ya sasa ya barabara ya kwenda zahanati ya kijiji cha Nyandage katani Nyanungu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime - Vijijini. (Na Mpigapicha Wetu)
----------------------------------------
Wakazi wa kijiji cha Nyandage kilichopo kata ya Nyanungu, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) wameiomba serikali iwajengee barabara ya kwenda zahanati ya kijiji hicho ili wapate urahisi wa kufikia huduma za matibabu.
Wakizungumza na Mara Online News kijijini hapo wiki iliyopita, viongozi wa kijiji hicho walilalamika wakisema ukosefu wa barabara hiyo umekuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi wanapohitaji kwenda kupata huduma kwenye zahanati hiyo.
"Ukosefu wa barabara ya kwenda zahanati ni kero kubwa, tumekuwa tukiandika na kuorodhesha barabara hiyo kama kipaumbele cha kijiji ila hakuna kinachofanyika,wakati wa masika tunazunguka umbali mrefu kwenda vijiji jirani.
"Hata kutokamilika kwa miradi ya maendeleo, ikiwemo nyumba ya Mganga Mkuu wa Zahanati ya Nyandage ni kutokana na ukosefu wa barabara ya kupitisha vifaa vya ujenzi.
“Tuliambiwa kuwa mkandarasi aliwahi kulipwa fedha kabla ya kazi lakini hakulima hii barabara,” alisema Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyandage, Mwita Kiya Rokomo.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngori kijijini Nyandage, Nyamsabi Marwa, alisema ukosefu wa barabara pia umekuwa ukikwaza mahudhurio ya wanafunzi shuleni kipindi cha mvua za masika.
Alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo ya wananchi, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Charles Marwa, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo lakini limeshawekwa kwenye mpango wa kutatuliwa.
“Tumeshaweka mkandarasi wa kulima na kukarabati barabara katika kata zote 26 za halmashauri yetu, maeneo mengine kazi imechelewa kwa kuwa mkandarasi ni mmoja, lakini tunamhamasisha aharakishe kazi ili hata wakazi wa Nyandage watatuliwe kero hiyo,” alisema Mhandisi Marwa.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
»Mvua yaharibu nyumba, miundombinu Musoma Mjini, baadhi ya watu wakosa makazi
»Taasisi ya Mwanzo Mpya yawanoa wanawake Tarime, yampongeza Rais Samia
»Namibia yamuapisha Rais wake wa kwanza mwanamke, Rais Samia ampongeza
»Serengeti: Mwenyekiti UVCCM Mara aunga mkono Serikali kufanikisha upatikanaji wa lishe mashuleni
No comments:
Post a Comment