
Na Mwandishi Wetu, Songea
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt Emmanuel John Nchimbi (pichani juu kulia), amehitimisha ziara yake ya siku tano mkoani Ruvuma, akisisitiza kuwa CCM itaendelea kuwa chama cha wanachama, kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wote na kuwa mtetezi wa wanyonge.
Balozi Nchimbi amesema kwamba katika kuendeleza nafasi yake kama taasisi imara inayohusika na uongozi wa nchi, CCM hakina budi kuendeleza misingi ya sera zake zinazolenga kubadilisha hali za maisha ya watu, kuendana na mahitaji ya nyakati na kuzingatia maslahi ya taifa.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi wa mji wa Songea, Ruvuma waliokusanyika kumpokea alipofika kufungua mradi wa kitega uchumi wa Tawi la CCM la Mshangano mjini Songea - Jumapili Aprili 6, 2025, ikiwa ni siku ya tano tangu alipoanza ziara hiyo Aprili 2, 2025.
Katika ziara hiyo aliyoifanya katika wilaya ya Tunduru, Namtumbo, Nyasa na hatimaye Songea Mjini, Balozi Nchimbi alitoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, kwa jinsi inavyotafsiri kwa vitendo na ufanisi, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, kupitia miradi ya maendeleo na huduma kwa wananchi.
Kiongozi huyo wa chama tawala - CCM, alitoa maelekezo kwa serikali kuendelea kusimamia na kubuni mipango inayolenga kuongeza matokeo chanya kwenye shughuli za uzalishaji mali, ikiwemo kilimo na madini, ili wakulima na wachimbaji madini waendelee kuzalisha kwa tija itakayoongeza pato la taifa na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, Balozi Nchimbi alitembelea na kutoa maelekezo mahsusi katika miradi kadhaa ya maendeleo na kimkakati inayotekelezwa na serikali kupitia wizara na taasisi zake, ikiwemo mradi wa uzalishaji mbegu chini ya Mamlaka ya Mbegu Nchini (ASA) na ujenzi wa Bandari ya Nyasa, kwa lengo la kuendelea kutafsiri utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Katika mikutano ya hadhara, pamoja na kusalimia wananchi maeneo ya Songea Vijijini, Mbinga na Songea Mjini, Balozi Nchimbi alipokea taarifa za utendaji wa kazi kutoka kwa viongozi wa chama na serikali, pamoja na maoni ya wananchi kuhusu changamoto zinazowakabili, kupitia kwa wabunge na wananchi moja kwa moja, kisha kutoa maelekezo ya kutatuliwa kwa kero hizo.
Balozi Nchimbi, ambaye amehitimisha rasmi ziara yake kwa kuondoka mkoani humo Jumatatu Aprili 7, 2025, alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wana-CCM na Watanzania kwa ujumla kwa ushirikiano wao na Serikali ya CCM katika kulinda tunu za taifa, ikiwemo amani na utulivu. Alitoa wito wa kuendeleza hali hiyo wakati nchi inapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment