
Kushoto ni Rais Dkt Samia Suluhu Hassan (kushoto), kulia ni Mbunge Jafari Wambura Chege.
-----------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Rorya
Wananchi wa wilaya ya Rorya, mkoani Mara sasa wana kila sababu ya kutabasamu, kufurahi na kushangilia, baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kutangaza tenda ya ujenzi wa barabara ya Utegi - Shirati kwa kiwango cha lami.
Kipande hicho cha barabara chenye urefu wa kilomita 27, kitaanza kujengwa kwa lami wakati wowote baada ya mkandarasi kupatikana kufikia mwishoni mwa Aprili mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Rorya, Mbunge Jafari Wambura Chege ambaye amesisitiza kuwa hiyo ni habari njema kwa wananchi wa jimbo hilo, alieleza furaha na shukrani zake kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
"Ninamshukuru sana Mhe. Rais wetu mpendwa, Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kusikia kilio cha watu wa Rorya, kunisikia mimi mwakilishi wao ambaye usiku na mchana nimekuwa nikiomba ili watu wangu wajengewe barabara hii kwa kiwango cha lami,” Mbunge Chege alisema katika mazungumzo na Mara Online News kwa simu jana.
Aliendelea” “Kwa tangazo [lililotolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)] la kupata mkandarasi, kusaini mkataba na kuanza kazi ya ujenzi, sisi watu wa Rorya hatuna cha kumlipa Mama [Rais Samia] zaidi ya kumpa kura za kishindo.”
Chege alisema ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umekuwa ukisubiriwa kwa miaka mingi sasa, na kwamba ukitekelezwa utaboresha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika wilaya ya Rorya.
“Awamu ya kwanza ya barabara hii itajengwa kwa kimolita 27 kutoka Utegi mpaka Shirati KMT, kisha itaendelea kwa awamu nyingine kwenda Kirongwe mpakani,” Chege alifafanua zaidi, akionesha matumaini na shukrani kwa Rais Samia kwa kuweka msukumo wa maendeleo katika jimbo hilo.
Kwa upande mwingine, wananchi wa Rorya wamepongeza hatua hiyo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia, wakisema ujenzi wa barabara hiyo utapunguza adha za usafiri na kuongeza fursa za kibiashara katika wilaya hiyo.
"Tunashukuru sana kwa hatua hii… Barabara hii itawezesha biashara za mazao na bidhaa mbalimbali kufika kwa urahisi kwenye masoko, na pia itarahisisha usafiri kwa wanafunzi na wagonjwa," alisema Mwalimu Jeremiah David.
No comments:
Post a Comment