
Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Kampuni ya Grumeti Reserves Ltd, Martha Baare.
----------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Serengeti
Martha Baare ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Grumeti Reserves Ltd, akiwa ni Mtanzania wa kwanza kupewa madaraka hayo katika kampuni hiyo ya kitalii na uhifadhi.
Kampuni ya Grumeti Reserves inamiliki hoteli kadhaa za kitalii zenye hadhi ya kimataifa mkoani Mara.
Kampuni hiyo inatoa mchango mkubwa kwa taifa kwa kusaidia shughuli za uhifadhi wa wanyamapori na maendeleo ya jamii katika vijiji vilivyo jirani na mapori ya akiba ya Ikorongo- Grumeti na Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Ikona, magharibi mwa Serengeti.
Baare anachukua nafasi ya Frank Law ambaye amefanya kazi kubwa ambayo imekuwa chachu ya mafanikio ya utendaji wa Kampuni ya Grumeti Reserves katika kipindi chake cha uongozi.
Kabla ya uteuzi huo, Baare alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu na Uhusiano wa Grumeti Reserves Ltd, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo hivi karibuni.
Kabla ya kuongozwa na Law, Grumeti Reserves Ltd pia iliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Graham Ledger, ambaye naye anasifika kwa kuchochea ukuaji mkubwa wa kampuni hiyo, ambapo hoteli zake zimekuwa zikitajwa kuwa hoteli bora duniani mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment