
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, akitubia Bunge la Jamhuri ya Angola jijini Luanda.
---------------------------------
Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, amepongeza juhudi za Rais wa Jamhuri ya Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, kudumisha uhusiano na urafiki wa muda mrefu baina ya nchi hizi mbili, na kwamba makubaliano yaliyofikiwa kwenye ziara yake nchini Angola, yataenda kuimarisha uhusiano wa kiuchumi.
“Kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi katika nchi zetu mbili, ikiwemo kwenye sekta za kilimo, utalii, viwanda na uchumi wa buluu, tumekubaliana kuimarisha mahusiano ya biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu.
“Ni kwa msingi huo, tumeshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya ushirikiano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Angola Private Investment and Export Promotion Agency (AIPEX), ikiwa ni hatua muhimu ya kukuza kiwango cha uwekezaji baina ya nchi mbili hizi,” alisema Rais Samia.
Alitoa pongezi hizo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa pamoja na mwenyeji wake, Rais João Manuel Gonçalves Lourenço katika Ikulu ya nchi hiyo iliyopo jijini Luanda.

Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake, Rais João Manuel Gonçalves Lourenço katika Ikulu ya Angola jijini Luanda.
------------------------------------
Aidha, katika kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo baina ya watu wa Tanzania na Angola na kuzidi kukuza biashara na uwekezaji, Rais Samia alitangaza kuwa Tanzania pia itaondoa sharti la kulipia visa ya utalii kwa raia wa Angola kuingia Tanzania, kama ambavyo Serikali ya Jamhuri ya Angola iliondoa sharti hilo kwa raia wa Tanzania kuingia nchini humo tangu mwaka jana.
Kwa upande wake, pamoja na mambo mengine, Rais Lourenço ameridhia mwaliko wa Rais Dkt. Samia kufanya ziara nchini Tanzania Julai 2026.
No comments:
Post a Comment