
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka (kulia), akipokea msaada wa magodoro 30 uliotolewa na mdau wa maendeleo, Dkt Wilson Mukama (kushoto), kwa ajili ya waathirika wa mvua mjini Musoma wiki iliyopita.
------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Musoma
Mdau wa Maendeleo, Dkt Wilson Mukama, ametoa msaada wa magodoro 30 kwa ajili ya baadhi ya familia zilizoathiriwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali katika mji wa Musoma hivi karibuni.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, alipokea na kukabidhi msaada huo kwa wahusika Alhamisi iliyopita.
“Tumepokea magodoro 30 kutoka kwa Dkt Mukama na tayari tumekabidhi kwa waathirika,” Chikoka aliiambia Mara Online News kwa simu juzi.
Dkt Mukama amekuwa miongoni mwa wadau waliotikia wito wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, wa kuunga juhudi zilizofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kusaidia familia zilizoathirika na maafa hayo ya mvua.
Siku chache baada ya maafa hayo kutokea, Rais Samia alitoa shilingi milioni 100 kusaidia familia zilizoathiriwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alikabidhi msaada huo wa Rais katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi, ambaye alitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia waathirika hao ili warejee katika maisha yao ya kawaida.
Mvua hiyo ambayo iliamabatana na upepo mkali iliezua paa za majengo ya makazi ya watu, biashara na taasisi mbalimbali, zikiwemo shule za msingi, kituo cha polisi, msikiti na kuharibu baadhi ya miundombinu ya umeme na barabara.
Wengine waliojitokeza kusaidia waathirika hao ni Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Mathayo, ambaye alitoa mitungi mikubwa ya gesi na majiko ya kupikia na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete, aliyewapatia mchele kilo 100.
No comments:
Post a Comment