Na Mwandishi Wetu
Mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi za Ubunge, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Udiwani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utaanza rasmi Mei 1, 2025.
Mchakato huo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana mjini Dodoma na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za maombi ya kuteuliwa kwa wagombea litakuwa ni la wiki mbili ambapo litakamilika Mei 15.
Kwa wana-CCM wanaogombea nafasi za Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, taarifa imesema kuwa watachukua na kurejesha fomu kwa Katibu wa CCM wa Wilaya husika.
Wanachama wanaogombea nafasi za Viti Maalum vya wanawake katika Bunge au Baraza la Wawakilishi kupitia kundi la UWT na makundi maalum, watachukua fomu na kuzirudisha kwa Katibu wa UWT wa mkoa unaohusika, taarifa imefafanua.
Nao wagombea wa Viti Maalum vya Wanawake katika Bunge au Baraza la Wawakilishi kupitia Jumuiya ya UVCCM watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa UVCCM Mkoa unaohusika.
Taarifa imeendelea kueleza kwamba kwa wagombea wa nafasi za Viti Maalum vya Wanawake kupitia Jumuiya ya Wazazi watachukua fomu na kuzirudisha kwa Katibu wa Wazazi Mkoa unaohusika.
Hali kadhalika, wanachama wanaogombea nafasi ya Diwani wa Kata kwa upande wa Tanzania Bara au Wadi kwa upande wa Zanzibar watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa CCM wa Kata/Wadi inayohusika, kwa mujibu wa taarifa.
Pia wagombea wa nafasi ya Udiwani Viti Maalum vya Wanawake watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa UWT wa wilaya husika.
Tanzania mwaka huu inafanya Uchaguzi Mkuu wa saba tangu iingie katika mfumo wa vyama vingi vya siasa hapo Julai 1, 1992.
Tangu kuanzishwa kwa mfumo huo wa vyama vingi, chama kikongwe cha CCM kimekuwa kikishinda chaguzi zote na kushika uongozi wa dola.
No comments:
Post a Comment