
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, akizungumza na mamia ya wakazi wa mji mdogo wa Nyamongo wilayani Tarime jana Aprili 26, 2025.
---------------------------------
Na Godfrey Marwa, Tarime
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya chama hicho tawala, itatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa mji mdogo wa Nyamongo, wilayani Tarime ili wapate maendeleo ya kiuchumi na kijamii
Balozi Dkt Nchimbi alitoa ahadi hiyo jana Jumamosi aliposimama kusalimia na kusikiliza kero za wananchi wa Nyamongo, wakati akiwa safarini kuelekea wilayani Serengeti kukamilisha ziara yake ya siku tano ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025.
Maombi yaliyowasilishwa na wananchi hao ni pamoja na kuipandisha Nyamongo kuwa na hadhi ya mji mdogo, kuwaimarishia huduma ya maji, kuwapatia wachimbaji wadogo wa dhahabu leseni, ajira kwa vijana na uharakishaji wa ujenzi wa VETA.
![]() |
Picha na Mara Online News |
"Changamoto hii ya mji mdogo nimeichukuwa, tutakwenda tuhangaike nayo ili siku moja mseme mwenzenu wa Mara amefika nalo pazuri. Nawapongeza kwa maendeleo - naona mnataka vitu vya maendeleo kama barabara za maana, hilo nalo tumelichukuwa," alisema Balozi Dkt Nchimbi.
Kuhusu maji, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kutenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya mradi wa kuhudumia vijiji vinne, na fedha nyingine zaidi za kupanua mradi ili uvifikie vijiji vyote 11 vilivyo jirani na mgodi huo.
"Suala la VETA mmsema speed (kasi) iongezeke, niwahakikishie kabla sijafika Serengeti nitakuwa nimetoa maelekezo kwa Waziri wa Elimu kuhusu kasi ya chuo hiki. Wachimbaji wadogo - nimemtafuta Waziri wa Madini ameniambia Mei 3, 2025 ndipo atakuwa hapa kugawa leseni za wachimbaji wadogo wadogo, nami nitafuatilia.
"Suala la fidia, nitazungumza na wizara zinazohusika, nimeambiwa baadhi ya fidia zimelipwa na zingine kuna mabishano, nitawambia waje mzungumze tumalizane nayo.
"Suala la mrabaha nimeambiwa lipo mahakamani, nilitaka niwaombe watu wa Nyamongo pamoja na kwamba documents (nyaraka) tutazitazama, mtakapokuwa mnazungumza na kujadiliana ni vizuri mkatengeneza utaratibu wa kupendana,” amesema Katibu Mkuu huyo wa CCM.
No comments:
Post a Comment