NEWS

Tuesday, 22 April 2025

Dkt Nchimbi aagiza wananchi Nyatwali walipwe fidia iliyobaki kupisha upanuzi Hifadhi ya Serengeti



Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, akizungumza na umati mkubwa wa wananchi mara baada ya kuwasili wilayani Bunda jana Aprili 22, 2025 kwa ziara ya siku tano mkoani Mara.
----------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Bunda

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt Emmanuel John Nchimbi, ameiagiza serikali kukamilisha fidia iliyobaki kwa wananchi wanaohamishwa kata ya Nyatwali, wilayani Bunda kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Balozi Dkt Nchimbi alitoa agizo hilo jana Aprili 22, 2025 wakati alipowasili na kuzungumza na wakazi wa Bunda, kuanza ziara yake ya siku tano ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025 mkoani Mara, akiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo, Patrick Chandi Marwa.

“Nilizungumza na Mhe. Rais kuhusu malipo ya fidia ya Nyatwali na ameridhia fedha hizo zilipwe, na mpaka sasa tayari asilimia 90 ya malipo ya fidia yameshalipwa, imebakia asilimia 10 tu ya fidia hizo,” alisema.

Kiongozi huyo wa chama tawala - CCM, alitumia nafasi hiyo kuwaelekeza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Waziri wa Fedha na Waziri wa Maliasili na Utalii kuhakikisha malipo hayo yanakamilishwa ndani ya wiki mbili zijazo.

Wakati huo huo, Balozi Dkt Nchimbi amewataka wananchi kuwakataa wanasiasa wenye viashiria vya kuruvuga amani ya nchi kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani nchini.

“Watanzania tuwakatae watu wa aina hiyo. Tusikubali amani yetu iliyodumu tangu uhuru ichezewe,” alisisitiza.

Kwa upande mwingine, amehimiza wananchi wenye sifa kuhakikisha kuwa wanajiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili waweze kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages