
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, akisalimiana na umati mkubwa wa wananchi mara baada ya kuwasili wilayani Bunda leo Aprili 22, 2025 kwa ziara ya siku tano mkoani Mara.
----------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Bunda
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, leo Aorili 22, 2025 amewasili na kupokewa na umati mkubwa wa wananchi wilayani Bunda, kwa ziara ya siku tano ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025, katika mkoa wa Mara.
Mkoa wa Mara unaundwa na wilaya sita; ambazo ni Bunda, Musoma, Butiama, Rorya, Tarime na Serengeti.
"Katibu Mkuu wetu atafanya ziara kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM mkoani kwetu kwa siku tano - tunamkaribisha sana," Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, ambaye ameongoza viongozi na wananchi kumpokea Balozi Dkt Nchimbi, ameiambia Mara Online News.

Chandi ametaja baadhi ya miradi ambayo kiongozi huyo wa kitaifa kutoka chama tawala ataikagua kuwa ni mradi wa maji ya Ziwa Victoria wa Rorya na Tarime unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 134 kutoka serikalini.
Mradi mwingine ni ujenzi wa barabara ya Tarime - Nyamongo - Mugumu/ Serengeti kwa kiwango cha lami, ambao pia inatekelezwa kutokana na mabilioni ya fedha yanayotolewa na serikali.
Chandi ametoa wito wanachama wa CCM na wananchi wa mkoa wa Mara kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwenye mapokezi na mikutano ya Balozi Dkt Nchimbi katika maeneo yote atakayopita wakati wa ziara yake hiyo katika mkoa huo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara,
Patrick Chandi Marwa.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati itakayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mkoa wa Mara uliopo Kanda ya Ziwa.
Miradi mingine mikubwa iliyotekelezwa mkoani Mara ni ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kwangwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, ambayo tayari imeanza kutoa huduma za kibingwa.
Pia, kuna mradi unaoendelea kutekelezwa wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) wilayani Butiama, ambacho kimeanza kudahili wanafunzi tangu mwaka jana.
Aidha, kuna mradi wa maji Mugango - Kiabakari - Butiama ambao Serikali ya Awamu ya Sita imeutekeleza kwa gharama ya shilingi bilioni 70.5 na kuwezesha wananchi zaidi ya 130,000 kuanza kupata huduma ya maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria.
Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa falsafa ya Rais Samia ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani.
Mradi mwingine ambao utekelezaji wake unaendelea ni upanuzi na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege Musoma ambao utasaidia kuharakisha maendeleo kiuchumi katika mkoa wa Mara uliojaaliwa kuwa na sehemu kubwa ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Hivyo, uboreshaji na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma utawezesha watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani kutua moja kwa moja katika mji wa Musoma kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo.
Katika orodha ya miradi mikubwa pia umo ule wa ujenzi wa wa barabara ya Nyamuswa - Bunda - Bulamba - Kisorya yenye urefu wa kilomita 121 ambao umekamilika kwa kiwango cha lami.
Utekezaji wa miradi hiyo na miingine ambayo haikutajwa katika habari hii inatarajiwa kuuwezesha mkoa wa Mara kuipiga hatua kubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mkoa wa Mara ndipo alikozaliwa gwiji wa siasa Tanzania na barani Afrika, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye aliendesha harakati za kuwang’oa wakoloni wa Kiingereza mwaka 1961.
Mkoa huo pia ndipo anakotoka Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira, ambaye tangu ujana wake amelitumikia taifa katika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Kwa Dkt Nchimbi, hii itakuwa ni fursa yake nyingine kuutembelea mkoa wa Mara kama Makamu wa Rais mtarajiwa baada ya Mkutano Mkuu wa CCM kumteua mapema mwa huu kuwa mgombea mwenza wa Rais Dkt Samia.
No comments:
Post a Comment