NEWS

Tuesday, 15 April 2025

RC Mara apokea awamu nyingine ya madawati ya CSR kutoka Barrick, Mbunge Waitara asema mgodi unawezesha maendeleo makubwa




Na Mwandishi Wetu, Nyamongo

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amepokea awamu nyingine ya madawati, viti na meza vinavyotengenezwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime.

RC Mtambi amepokea madawati 310 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi, viti na meza 295 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari.



Madawati, meza na viti hivyo vinatengenezwa kupitia mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamiii (CSR) wa mgodi wa huo ambao unaoendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

“Nimefarijika kupokea madawati haya, nimeyakagua, ni mazuri na yana ubora unaotakiwa,” Kanali Mtambi alisema katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika jana Jumatatu kwenye viwanja ya Shule ya Sekondari Ingwe iliyopo katika mji mdogo wa Nyamongo.

Kanali Mtambi akikagua madawati.


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, akizungumza katika hafla hiyo.
-----------------------------------

Kanali Mtambi aliupongeza mgodi wa North Mara kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 898 utakapokamilika.

Hafla ya kukabidhi madawati hayo ilishuhudiwa na wanafunzi, walimu na viongozi wa kijamii kutoka maeneo yaliyo jirani na mgodi huo.

Wiki chache zilizopita, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele alipokea awamu ya kwanza ya mdawati hayo ya mradi huo.

Wakandarasi wazawa wanne wamepewa kazi ya kutengeneza madawati hayo ili kazi ikamilike haraka. Takriban madawati 900 yanayohusisha pia viti na meza yanatarajiwa kutengenezwa chini ya mradi huo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Noth Mara, Apolinary Lyambiko, alisema utengenezaji wa madawati hayo ni moja wa miradi 101 ambayo utekelezaji wake unaendelea katika Halmashauri ya Wiaya ya Tarime kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni tisa zilizotolewa na mgodi huo kupitia mpango wake wa CSR.


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kulia), akiteta jambo na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko katika hafla ya makabidhiano ya madawati hayo.
------------------------------------

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, alisema kampuni ya Barrick inafanya kazi nzuri katika kuwezesha na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika jimbo hilo.

Hivyo, Waitara alisisitiza msimamo wake wa kuunga mkono uwekezaji wa kampuni ya Barrick katika mgodi huo akisema una faida kwa wananchi na taifa kwa ujumla.


Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, akizungumza katika hafla hiyo.
--------------------------------

“Huyu ni mwekezaji, anafanya shughuli zake na anafanya mambo makubwa kuwezesha makundi mbalimbali ya wananchi. Mbunge akisema mgodi unafanya kazi nzuri inakuwa shida,” alisema mbunge huyo kutoka chama tawala - CCM.

Alisema mgodi huo umetoa mabilioni ya fedha, yakiwemo ya ushuru wa huduma kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, lakini pia gawio la mrabaha kwa vijiji vitano.

Waitara aliongeza kuwa mahusiano kati ya mgodi huo na jamii inayouzunguka yameimarika zaidi kwa sasa ukiliganisha na miaka ya nyuma. “Tumeboresha mahusiano, na mimi kama mbunge ninaunga mkono mgodi na serikali,” alisema.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages