
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara,
Patrick Chandi Marwa.
----------------------------------
Na Mwandishi Maalumu
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, amewatahadharisha wanachama wa chama hicho kutochafuana wakati wa kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika Uchaguzi Mkuu unaotajiriwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
“Dirisha la kuchukua fomu litakuwa wazi kuanzia mwanzoni mwa mwezi ujao, wana-CCM wajitokeze kuchukua fomu kwa nafasi za ubunge na udiwani, na ratiba izingatiwe kama ilivyotolewa,” Chandi aliiambia Mara Online News kwa njia ya simu Jumamosi iliyopita.
Aliwata makada wa CCM ambao wanataka kuomba uteuzi wa kugombea nafasi hizo kutofanya siasa za kuchafuana ili kuendelea kulinda hadhi na heshima ya chama hicho tawala nchini.
“Kusiwepo na tabia za kuchafuana, kwa kutoleana matusi, kejeli, fitina au chuki,” alionya bosi huyo wa CCM mkoa wa Mara.
Hivyo, alihimiza suala la nidhamu na ustaarabu kutamalaki katika kipindi chote cha uchukuaji na urejeshaji fomu za kuomba uteuzi.
“Wachukue fomu kistaarabu na waendelee kulinda heshima ya CCM, mwisho wa siku waamuzi watakuwa wanachama,” alisisitiza Chandi.
Zoezi la kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi za ubunge na udiwani ndani ya CCM litaanza Mei 1, 2025, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla.
Mkoa wa Mara unatarajiwa kushuhudia mchuano mkali katika baadhi ya majimbo, yakiwemo Tarime Vijijini, Mwibara, Rorya, Bunda Mjini, Tarime Mjini, Serengeti na Musoma Mjini.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
»Nyansaho Foundation yawajengea walimu nyumba tatu Sekondari ya Musati wilayani Serengeti
»Dkt Mukama atamani Mara iendelee kuwa kinara UMITASHUMITA, achangia mashindano shilingi milioni 4
»Mgodi wa Barrick North Mara watenga bilioni 4.687/- nyingine za miradi ya kijamii Tarime Vijijini
»RC Mara apokea awamu nyingine ya madawati ya CSR kutoka Barrick, Mbunge Waitara asema mgodi unawezesha maendeleo makubwa
No comments:
Post a Comment