NEWS

Tuesday, 15 April 2025

Mkuu wa Mkoa aridhishwa kasi ya ujenzi wa barabara ya lami Mogabiri - Nyamongo



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati mbele), akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mogabiri – Nyamongo kwa kiwango cha lami Ijumaa iliyopita. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kushoto) na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe (kulia). (Picha na Mara Online News)
-----------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 25 inayoanzia Mogabiri hadi Nyamongo wilayani Tarime.

"Nimekagua barabara hii ya Mogabiri-Nyamongo, kasi kwa sasa inaridhisha, naona mkandarasi umerudi na nguvu mpya na kasi mpya, muendelee na kasi hiyo hiyo, tunataka ikamilike kwa wakati," Kanali Mtambi alisema mara baada ya kukagua mradi huo Ijumaa iliyopita.

Barabara hiyo inajengwa na mkandarasi mzawa Nyanza Road Works, huku Serikali ya Tanzania ikiwa imetoa mabilioni ya fedha kugharimia mradi huo, ikiwa ni sehemu ya kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya kijamii kwa wananchi.

Barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Tarime - Mugumu yenye urefu wa kilomita 87.14 ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwanga cha lami unaelezwa kuwa utasaidia kuharakisha maendeleo ya sekta za utalii na kilimo, pamoja na huduma za kijamii katika wilaya za Tarime na Serengeti.

Watalii wengi wanaozuru nchini kupitia mpaka wa Sirari wanatumia barabara hiyo wanapotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti, mbali ya kuwa tegemeo kubwa kwa wananchi wa wilaya hizo mbili.

"Barabara hii ni muhimu kwa maendeleo ya utalii, inaenda kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti, itakuwa ni neema kwa angle (kona) zote," alisema Kamali Mtambi.

Jambo la kufurahisha ni kwamba tatari wananchi wameruhusiwa kutumia sehemu ya barabara hiyo wakati ujenzi ukiendelea.

Kwa mujibu wa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe, ujenzi wa barabara hiyo ya Mogabiri - Nyamongo utagharimu shilingi bilioni 34.6 hadi kukamilika kwake.

Mhandisi Maribe alisema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuufungua mkoa huo kwa barabara za lami, huku akitaja baadhi ya barabara za kimkakati zinazojengwa na zitakazojengwa kwa kiwango cha lami.

Mbali na ujenzi wa barabara hiyo ya Tarime - Mugumu/Serengeti, alitaja barabara nyingine kuwa ni Sanzate - Makutano - Natta ambapo mkandarasi yupo kazini, na Musoma - Busekela yenye urefu wa kilomita 92.

Alitaja barabara nyingine kuwa ni inayoanzia Mika - Utegi - Shirati mpaka Kirongwe yenye urefu wa kilomita 56.4, ambayo tenda yake tayari imekwisha kutangazwa na kazi itaanza na kilomita 27 kutoka Utegi hadi Shirati.

RC Mtambi aliitaka TANROARDS kusimamia kwa karibu utekelezaji wa ujenzi wa barabara za lami katika mkoa huo ili ziweze kukamilika kwa wakati.

“Mhe. Mkuu wa Mkoa, hizi barabara zote zikifunguka mkoa wa Mara utakuwa umefunguka na uchumi wa mkoa utazidi kukua,” Mhandisi Maribe alisema.

Awali, Kanali Mtambi alitembelea na kukagua mradi wa uboreshaji na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma, ambao pia unatarajiwa kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha utalii.

Mkoa wa Mara umebarikiwa kuwa na fursa nyingi za kiuchumi kama vile Hifadhi ya Taifa Serengeti, Ziwa Victoria, madini na ardhi ambayo inastawisha mazao mbalimbali, ikiwemo kahawa aina ya Arabica ambayo inafanya vizuri katika soko la dunia.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages