NEWS

Saturday, 5 April 2025

TANAPA yaweka vipaumbele katika bajeti yake ya mwaka 2025/2026




Na Andrew Mbai, Mto wa Mbu

Menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) inayoongozwa na Kamishna wa Uhifadhi, Juma Nassoro Kuji, imeweka vipaumbele muhimu katika bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2025/2026, ili kuboresha shughuli za uhifadhi na utalii nchini.

Vipaumbele hivyo vimewekwa katika kikao kazi cha Menejimenti ya TANAPA kilichojadili maandalizi ya mwisho ya bajeti ya shirika hilo kwa mwaka mpya wa fedha wa 2025/2026.

Kikao hicho kilifanyika jana Aprili 04, 2025, katika Hifadhi ya Taifa Manyara.


Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Juma Nassoro Kuji, akikagua gwaride la Askari wa Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa Manyara.
-------------------------------

Akizungumza na washiriki wa kikao, Kamishna Kuji alieleza dhima ya TANAPA katika kutengeneza bajeti inayoangazia vipaumbele vinavyotatua changamoto na kuboresha utendaji na utekelezaji wa majukumu ili kufikia malengo ya shirika hilo na taifa kwa ujumla.

“Mwaka ujao wa fedha wa 2025/2026 tunaweka mkazo katika kuongeza nguvu kwenye shughuli za ulinzi na usalama wa hifadhi, kuendelea kuboresha miundombinu ya utalii, kuboresha upatikanaji na uboreshaji wa vitendea kazi, kama vile kupata magari kwa ajili ya doria na kukarabati yenye uhitaji huo.” alisema Kamishna Kuji.

Pia, alisisitiza kutengeneza bajeti itakayolenga kutoa msukumo katika uanzishaji wa mazao mapya ya utalii ili kuongeza mapato ya TANAPA na taifa, ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za uhifadhi, matumizi ya teknolojia, utatuzi wa migogoro kati ya wanyamapori (wakali na waharibifu) na binadamu sanjali na kuboresha maslahi kwa watumishi.

Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya TANAPA wilipata fursa ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya shirika hilo inayoendelea ya mwaka 2024/2025, ambapo walibainisha maeneo ya msingi ambayo yametekelezwa kwa ufanisi, ikiwemo kuhamasisha Watanzania kuchangamkia fursa ya kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea Hifadhi za Taifa na Vituo vya Malikale vilivyokasimishwa kwa TANAPA.

Sambamba na hilo pia, kamati hiyo ilitaja maeneo mengine ya kuweka kipaumbele kuwa ni pamoja na kuendelea kufanya maboresho ya miundombinu ya utalii na utawala, ikiwemo matengenezo ya barabara hifadhini, ujenzi wa malango ya utalii na hosteli zinazotumiwa na wanafunzi wanapotembelea Hifadhi za Taifa, udhibiti wa mimea vamizi, wanyamapori wakali na waharibifu, utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa jamii na utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo.

Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Sekela Mwangota, ambaye ndiye Katibu wa Kamati ya Bajeti ya TANAPA alielezea namna bajeti mpya ilivyoandaliwa.

“Uandaaji wa mapendekezo ya bajeti ya shirika kwa mwaka wa fedha 2025/2026 umezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020, Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali wa Mwaka 2025/2026, Mpango Mkakati wa Shirika, Sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali za nchi, vipaumbele vya shirika na nchi pamoja na maelekezo mahsusi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanayolenga kuboresha ustawi wa jamii ya Watanzania” alisema Kamishna Mwangota.

Mapendekezo ya Bajeti ya TANAPA kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yatawasilishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi kwa ajili ya uchambuzi na idhini kabla ya kuanza kutumika rasmi Julai 1, 2025.

TANAPA inaendelea kutekeleza majukumu yake ili kuhakikisha kuwa uhifadhi endelevu wa maeneo yote yaliyotengwa kuwa Hifadhi za Taifa nchini unaimarika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages