NEWS

Wednesday, 2 April 2025

Wananchi washangilia ujio wa Gridi ya Taifa ya Maji



Rais Dkt Samia Suluhu Hassan (kulia), na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, siku ya uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Maji kwenye Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Maji 2025.
-------------------------------------

Na Mwandishi Wetu

Maelekezo yaliyotolewa hivi karibuni na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuanzishwa Gridi ya Taifa ya Maji, yamepokewa kwa shangwe na wananchi mbalinmbali wakisema hatua hiyo itakuwa ni tiba ya tatizo la uhaba wa maji nchini.

Wananchi kadhaa waliohojiwa na gazeti hili wamesema rai ya Rais Samia ya kushughulikia tatizo sugu la ukosefu wa maji nchini imekuja wakati muafaka, hasa kutokana na ongezeko la watu, mabadiliko ya tabianchi na migogoro inayosababishwa na rasilimali hiyo miongoni mwa wananchi, hasa wakulima na wafugaji.

Wakati wa uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Maji 2025 uliofanyika jijini Dar es Salaam Machi 22, mwaka huu, Rais Samia aliiagiza Wizara ya Maji kuanzisha Gridi ya Taifa ya Maji yenye lengo la kuwa na vituo vingi vya kupokelea maji kutoka vyanzo mbalimbali nchini kwa kuweka vituo vya kanda vitakavyotumika kusambaza maji nchi nzima.


Rais Samia akipokea Tuzo ya Kinara wa Maji Afrika (The PANAFRICAN Water, Sanitation and Hygiene Champion Award) kutoka kwa Taasisi ya WaterAid UK ya nchini Uingereza wakati wa hafla ya Kilele cha Wiki ya Maji 2025 na Uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Maji 2002 jijini Dar es Salaam.
----------------------------------------

Kwa muktadha wa miundombinu ya maji, Gridi ya Taifa ya Maji inamaanisha muunganiko wa mtandao wa vyanzo mbalimbali vya maji, kama vile mabwawa, mabomba, pampu na menejimenti ya mifumo iliyoundwa, ili kuhakikisha upatikanaji wa maji kimkoa hadi kufikia ngazi ya vijiji kwa ajili ya matumizi katika kilimo, viwanda na shughuli nyingine za uzalisaji mali ili kukuza uchumi.

“Ninaagiza ianzishwe Gridi ya Maji ya Taifa ili yaweze kufika katika maeneo yote nchini na kumaliza changamoto ya uhaba wa maji. Agizo hili lifanyiwe kazi mara moja,” alisema Rais Samia alipozindua Sera ya Taifa ya Maji 2025.

Hatua hiyo muhimu, itashuhudia uwepo wa Gridi ya Maji ya Taifa ambayo itahusisha maziwa na mito mikubwa iliyopo nchini.

“Maana ya Gridi ya Maji ya Taifa itakuwa ni maji kutoka maziwa na mito mikubwa, na mfano mzuri ni maji kutoka Ziwa Victoria yaliyofika Tabora Mjini na Igunga ambako hakuna vyanzo vikubwa vya kutosha,” anasema mtaalamu mmoja kutoka Wizara ya Maji nchini

Tanzania ambayo ni moja ya nchi chache za Afrika zilizopiga hatua ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi wengi ambapo ifikapo Desemba 2025 lengo litakuwa asilimia 85 kwa upande wa vijijini na asilimia 95 kwa maeneo ya mijini.

Serikali ya Tanzania katika awamu zote za uongozi imekuwa mstari wa mbele kuwapunguzia wanawake mzigo wa kutafuta maji maeneo ya vijijini ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta rasilimali hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu.

Kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, jitihada kubwa zimefanyika katika kuwekeza katika sekta ya maji kwa kuanzisha miradi mbalimbali ili upatikanaji maji uwe endelevu kulingana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages