
Charles Hillary enzi za uhai
Na Mwandishi Wetu
Nguli wa tasnia ya utangazaji, Charles Hillary, 66, amefariki dunia jana jijini Dar es Salaam wakati akipelekwa Hospitali ya Mlonganzila kwa matibabu.
Hillary alikuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu alipoteuliwa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi mwaka 2021.
Taarifa kutoka Ikulu ya Zanzibar ilieleza kwamba bingwa huyo wa utangazaji aliugua ghafla ndipo akakimbizwa kwenda Hospitali ya Mlonganzila.
Alijiunga na fani ya utangazaji mwaka 1981 hadi mwaka 1994 alipoajiriwa na iliyokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (sasa Shirika la Utangazaji Tanzania) ambako alijipatia umaarfu, hasa katika utangazaji wa michezo ya mpira wa miguu.
Pia, alifanya kazi RadioOne Sterio kabla ya kujiunga na redio za kimataifa – Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na Sauti ya Ujerumani (DW), ambako pia alipata fursa za kukonga nyoyo za wasikilizaji kwa utangazaji wake mahiri.
Baadaye Charles Hillary alirudi nyumbani Tanzania na kujiunga na vyombo vya habari vya Azam kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar.
Kifo cha nguli huyo wa utangazaji kimewashtua watu wengi waliomfahamu, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye katika taarifa yake jana alisema Tanzania imempoteza mwanahabari mashuhuri aliyekuwa mwalimu kwa wanahabari wengine wanaochipukia.
Mwandishi mbobezi wa Shirika la Utangazaji Tanzania, Lugenzi Kabale, alimweleza Hillary kwamba alikuwa mtu aliyekuwa hana majivuno na alipenda sana kuchanganyika na watu wa kila aina.
“Hakuwa mjivuni na aliwapenda watu ndiyo maana alikuwa maarufu kwa wasikilizaji wake,” alisema Kabale jana alipopata habari za kifo cha nguli huyo wa utangazaji.
Naye mwandishi mwingine mbobezi wa Tanzania, Alpha Isaya Nuhu, alimweleza marehemu kwamba alikuwa ni mtu mnyenyekevu aliyejua mambo mengi wakati wa utangazaji wake.
“Saut nzito ya Charles katika utangazaji ilibeba mamlaka na watu wengi walikuwa wakimsikiliza kwa makini alipokuwa akisoma taarifa ya habari enzi zake,” alisema Nuhu ambaye alimfahamu Hillary tangu miaka ya 1980.
No comments:
Post a Comment