
Mbunge wa Jimbo la Butiama,
Jumanne Sagini.
Na Mwandishi Maalumu
Huwezi kuzungumzia maendeleo ya jimbo la Butiama, mkoani Mara bila kutaja jina la Jumanne Sagini. Hii ni kutokana na maendeleo makubwa ya kisekta yaliyopatikana chini ya uongozi wake baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge jimbo hilo mwaka 2020.
Maendeleo hayo ni matunda ya jitihada kubwa zilizofanywa na Mbunge Sagini kwa kuomba na kushawishi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi thabiti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa fedha za kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Lakini pia, hatua hiyo ya kuibadilisha Butiama kimaendeleo imechangiwa na ushauri ambao Mbunge Sagini amekuwa akipata kutoka kwa madiwani, viongozi wa chama tawala – CCM na watendaji wa serikali katika kusukuma na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.
Sekta ya elimu
Katika kipindi cha miaka mitano ambayo Mbunge Sagini amekaa madarakani, jimbo la Butiama limepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu. Mfano, shule za msingi 12 na sekondari nane zimeanzishwa ili kuwapunguzia wanafunzi adha za kutembea umbali mrefu na msongamano madarasani, hali ambayo imechangia kuongeza ufaulu.
Mafanikio mengine ni ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT), pamoja na Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA).
Pia, ujenzi wa Ofisi ya Uthibiti Ubora wa Shule, madarasa mawili katika Shule ya Msingi Kwisaro, mabweni yalioungua katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Chief Ihunyo na mabweni mawilli katika Shule ya Sekondari Bumangi baada kukumbwa na janga la moto.
Sagini anaongeza kuwa umefanyika ukarabati wa Shule kongwe ya Sekondari Kiagata kwa gharama ya shilingi milioni 90, ukarabati na ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Kiabakari, huku akichangia vitanda katika Shule ya Sekondari Mkono na madawati Shule ya Msingi Kiagata.
“Vilevile, tumejenga bweni la wasichana katika Sekondari ya Kyanyari na madarasa mawili katika Shule ya Msingi Nyamihuru,” anasema Mbunge Sagini katika mazungumzo na Sauti ya Mara jimboni Butiama hivi karibuni.
Michango mingine aliyotoa ni ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Nyandewa na shilingi milioni 1.5 za ujenzi wa shule shikizi Kyankoma iliyopo Nyamimange.
Lakini pia, Mbunge Sagini amekuwa akitoa misaada ya vifaa vya shule na nauli kwa wanafunzi wanaochaguliwa kwenda kusoma katika shule, vyuo vya kati na vikuu vikuu nje ya Butiama.
Sekta ya afya
Sekta ya afya nayo haikuachwa nyuma, kwani zahanati 16, vituo vya afya vitatu na Hospitali mpya ya Wilaya ya Butiama vimejengwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Mbunge Sagini.
Zaidi ya hapo, huduma za Mionzi X-ray na Utra Sound ambazo hazikuwepo zimeanzishwa na upatikanaji wa dawa umeongezeka kutoka asilimia 65 hadi 85, huku idadi ya watumishi wa afya nayo ikipanda kutoka 236 mwaka 2020 hadi 313 mwaka 2023.
“Mbali na mafanikio hayo, nimekuwa nikitumia fedha zangu binafsi kuwawezesha wananchi mbalimbali kwenye changamoto za matibabu,” anasema Sagingi.
Sekta ya maji
Mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya maji wakati wa uongozi wa Mbunge Sagini ni pamoja na ujenzi na uboreshaji wa miradi ya maji kwa ghatama ya shilingi bilioni 5.3.
“Tumefanikiwa pia kukarabati lambo la maji la Bukabwa kwa ajili ya matumizi ya mifugo na binadamu,” anaongeza.
Sekta ya barabara
Mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta hii ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Kitaramanka – Matongo, Sirorisimba – Mirwa na ufunguzi wa barabara mpya kadhaa, ikiwemo ya Kizaru.
Sagini anasema yamefanyika pia matengenezo ya barabara na makalvati, ambapo alifuatilia zikapatikana shilingi bilioni 5.866 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, sehemu korofi, matengenezo maalum, ujenzi wa makalvati na ufunguzi wa barabara mpya.
Kilimo na ufugaji
Katika sekta hii yameshuhudiwa mafanikio makubwa kuwahi kutokea katika historia ya jimbo la Butiama kutokana na msukumo wa Mbunge Sahini.
Anataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni usambazaji wa miche ya mkonge katika vijiji vya Buswahili, Nyankanga na Kitasakwa, usambaza mbegu za pamba tani 60 na viuatilifu vya zao hilo katika kata 11.
Kwa upande mwingine, vikundi vya wakulima vimegawiwa mbegu bora za mhogo katika tarafa za Makongoro na Kiagata, huku mbegu za mhogo kinzani dhidi ya magonjwa ya batobato kali na mchirizi zikisambazwa kwa wakulima.
Hali kadhalika, miche ya kahawa imesambazwa katika vijiji vya Biatika, Butiama, Buhemba, Matongo na Kinyariri. Pia, viuatilifu aina ya Banofos EC 720 vimesambazwa kwa wakulima wa mahindi katika vijiji 59.
Mbunge Sagini anataja mafanikio mengine kuwa ni ujenzi wa majosho ya kuogeshea mifugo katika maeneo ya Ryamgabo, Kirumi na Bisumwa.
Lakini pia, yameanzishawa mashamba darasa ya malisho ya mifugo katika maeneo ya Nyabange na Mwibagi, pamoja na ununuzi wa pikipiki 22 za maafisa kilimo wa kata, vijiji na wilaya ili kurahisisha huduma za ugani kwa wakulima.
Huduma nyingine za kijamii
Mbunge Sagini anasema katika kipindi chake cha uongozi, vitongoji 30 vimeunganishiwa umeme kupitia REA, na taa za barabarani zimewekwa katika kila senta ndani ya Butiama.
Licha ya hayo, wamefanikisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja B' ngazi ya Wilaya, Ofisi ya Uhamiaji Wilaya, ukamilishaji wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Ujenzi mwingine ni nyumba za Katibu Tawala wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama na ujenzi wa nyumba za askari magereza Kiabakari.
“Nimeweza pia kuanzisha ujenzi wa vibanda vya Pumzika na Sagini ambavyo vinaendelea kujengwa katika kata zote na senta maarufu katika jimbo la Butiama. Pia, nimetoa saruji mifuko 650 awamu ya kwanza katika kata 10,” anasema mbunge huyo.
Sagini ameweza kuweka msukumo pia katika uimarishaji wa mifumo ya haki, usalama na miundombinu ya utawala wilayani Butiama.
Maendeleo ya taasisi za kidini
Kwa upande wa dini, Mbunge Sagini ameweza kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki Nyabange na Bisumwa, Msikiti wa BAKWATA Mkoa wa Mara, Msikiti wa Mkiringo Kata ya Nyankanga na Msikiti wa Bisarye.
Amechangia pia ujenzi wa upanuzi wa Kanisa Katoliki Bisarye Kata ya Masaba, Kanisa la SDA Bisarye Kata ya Masaba na Kanisa jipya la Masalia ya Mitume (P.R.A.C.I) katika kijiji cha Nyabange katani Nyankanga.
Pia, amechangia ukarabati wa Msikiti wa Kiabakari Kata ya Kukirango, ujenzi wa Msikiti wa Kiagata, saruji mifuko 50 kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa Katoliki Kongoto, matofali 1,000 na saruji mifuko 30 ya ujenzi wa kanisa lililopo Kitasakwa.
Kuchangia maendeleo CCM
Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge Sagini amekuwa nguzo muhimu katika michango na utekelezaji wa Ilani ya chama hicho tawala.
Pamoja na mambo mengine, ameweza kulipa posho na kuwawezeaha wajumbe wa Halmashauri ya Wilaya kushiriki katika ziara ya viongozi CCM Mkoa wa Mara, lakini pia ziara za viongozi wa UWT Wilaya ya Butiama na Mkoa wa Mara.
Vilevile, ameweza kugharimia malipo ya Bima ya gari la CCM Wilaya ya Butiama, kutoa fedha kwa ajili ya matumizi ya Ofisi ya CCM Wilaya ya Butiama na kuwawezesha wananchama na viongozi wa CCM wilaya kuhudhuria mikutano ya viongozi wa kitaifa.
“Lakini pia, nimekuwa nikiwawezesha makatibu wa CCM wa matawi na wilaya kufanya vikao, kuwezesha vikao vya Halmashauri Kuu na kufadhili kambi na makongamo ya UVCCM Wilaya,” anasema Sagini.
Amewezesha pia matengenezo ya gari la CCM na kutoa gari kwa ajili ya huduma za chama hicho, pamoja na kuwezesha vikao vya chama katika vijiji vyote 59.
“Sambamba na hayo, nimekuwa nikihudhuria vikao mbalimbali vya chama kadri vinavyoitishwa, huku nikitoa malipo ya posho kwa viongozi wa ofisi ya CCM Wilaya ya Butiama, mchango kwa UVCCM Mkoa wa Mara katika kongamano la kumpongeza Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan,” anaongeza Sagini ambaye kwa sasa ni Naibu wa Waziri wa Katiba na Sheria .
Posho nyingine ambazo amekuwa akitoa ni kwa viongozi wa CCM wa kata, kuwezesha ziara ya Madiwani wa Viti Maalum Wilaya na kikao cha Baraza la Wazazi Wilaya ya Butiama.
Pia, kusimamia na kuwezesha Kamati ya Siasa ya Wilaya, wenyeviti wa CCM Kata, makatibu wa siasa na uenezi CCM Kata katika mwaliko Bungeni na kuwezesha vikao vya chipukizi CCM Wilaya.
Hali kadhalika Mbunge Sagini ameweza kununua viti 20 kwa ajili ya CCM Kata ya Buswahili na kugawa majiko na mitungi ya gesi kwa wajumbe wa Halmshauri Kuu Wilaya na viongozi wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mara.
Lakini pia, Sagini amegawa majiko na mitungi ya gesi kwa viongozi wa UWT ngazi ya kata na kuchangia viti 50 mradi wa UVCCM Nyamimange, saruji mifuko 50 ya ukarabati wa ofisi ya CCM Kongoto na ofisi ya Kitaramanka.
Sanaa na michezo
Kwenye sekta ya sana ana michezo, Mbunge Sagini kwanza ni mlezi wa vikundi vyote vya sanaa wilayani Butiama.
Lakini pia, amesaidia uanzishwaji na usajili wa Chama cha Soka Wilaya ya Butiama (BFA) na kugharimia mashindano na matamasha ya michezo kila mwaka ikiwemo soka, mpira wa pete, kufukuza kuku, mbio za baiskeli, ngoma za asili na muziki.
“Nimefadhili ligi ya vijana wa Kiabakari, kuunganisha kikundi cha EGUMBA na kushinda Tamasha la Tulia Ackson, pamoja kutoa zawadi za mashindano ya Sagini Cup kila mwaka,” anasema.
Ukaribu na wananchi
Mbunge Sagini amekuwa mfano mzuri wa kiongozi wa kusikiliza na kushughulikia changamoto za wananchi bila ubaguzi.
Amekuwa akifanya ziara za kuwatembelea wananchi majumbani kuwajulia hali na kuwasaidia mahitaji ya afya na elimu.
Vilevile, kuhudhuria shughuli za kijamii kama harambee za madhehebu ya dini, jamii, taasisi na vikundi, kushirikia na jamii bega kwa bega katika kuhani misiba.
Aidha, aliwapa motisha vijana wa Butiama walioshiriki matembezi ya hiari kwa miguu kutoka wilayani Butiama hadi mkoani Mwanza.
Mbunge Sagini pia alijitolea kugharimia posho za madiwani aliowaalika bungeni jijini Dodoma, lakini pia kuwezesha vikao vya maafisa watendaji wa vijiji wilayani Butiama.
Kwa upande mwingine, Sagini ameweza kukipatia Kikundi cha Wanawake Wilaya ya Butiama fedha za kukuza mtaji wao na kufadhili kila mwaka wiki ya kumbukizi ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere inayoratibiwa na Makumbusho ya Butiama.
“Nimeweza pia kutoa msaada wa mabati kwa Mzee Watiri Warioba aliyeshikiliwa miaka 30 gerezani na kuachiwa mwaka 2021 baada ya kubainika hana kosa, pamoja na msaada wa mabati 28 kwa mhitaji mwenye ulemavu Nyakwibote na mabati matano kwa mwingine mwenye ulemavu katani Kiagata,” anasema Mbunge Sagini.
Anaongeza: “Vilevile, nimeweza kuwapambania mpaka kufanikisha kupandishwa vyeo watumishi 1,644, hivyo kuinua motisha kwa watendaji, na nimefuatilia watumishi wakalipwa malimbikizo ya mishahara yao, ikiwa ni asilimia 60 ya fedha zilizokuwa zikidaiwa kama malimbikizo.”
Kwa ujumba, jimbo la Butiama limepiga hatua kubwa ya maendeleo ya kisekta chini ya uongozi madhubuti wa Mbunge Jumanne Sagini.
Ni wazi kuwa bado Sagini anahitajika ili kukamilisha safari ya maendeleo. Hivyo, wana-Butiama wana kila sababu ya kusimama naye kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa ajili ya kuendeleza ndoto ya “Butiama Mpya Inawezekana Kila Mmoja Akitimiza Wajibu Wake”.
No comments:
Post a Comment