NEWS

Tuesday, 13 May 2025

Wachimbaji madini, wafanyabiashara wammwagia sifa Rais Samia kwa kuendeleza sekta ya madini


Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akiongoza msafara wa maandamano ya amani ya wachimbaji madini na wafanyabiasha ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya madini. Maandamano hayo yalifuatiwa na kongamano lililofanyika mji mdogo wa Katoro mkoani Geita mwishoni mwa wiki iliyopita kujadili maendeleo kwenye tasnia ya madini.      
      ---------------------------------------------
 
Na Mwandishi Wetu

Mamia ya wachimbaji na wafanyabiashara ya madini mkoani Geita wamesifu jitihada za serikali za kuboresha sekta hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Wamesema serikali imeleta mageuzi katika tasnia ya madini kwa kuweka mazingira rafiki ya uchimbaji na ufanyaji biashara wa raslimali hiyo ili iweze kuchangia maendeleo ya taifa.

Wachimbaji na wafanyabiashara hao walimwaga sifa hizo kwenye kongamano lililofanyika mwishoni mwa wiki katika mji mdogo wa Katoro mkoani Geita ambalo lilikuwa ni kusanyiko la kumpongeza Rais Samia kwa kuwa mstari wa mbele kukuza sekta ya madini ili itoe mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Geita (GEREMA), Titus Kabuo, alisema wachimbaji wa madini wanamshukuru Rais Samia kwa utashi wake wa kisiasa wa kujenga mazingira mazuri kwa uchimbaji madini na biashara inayoambatana na raslimali hiyo ili kukuza vipato vya watu walioajiri kwenye sekta hiyo.

Rais wa Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, alisema miaka minne ya uongozi wa Rais Samia imeshuhudia mageuzi makubwa ya upatikanaji leseni kwa wachimbaji, jambo lililoleta hamasa ya vijana wengi kujiingiza katika ajira ya uchimbaji.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde aliorodhesha mafanikio 16 yaliyopatikana katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mchango kwenye Pato la Taifa kufikia asilimia 10.1.

Mafanikio mengine ni ununuzi wa dhahabu kupitia Benki Kuu, kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli kuelekea lengo la kukusanya shilingi trilioni moja na kupatikana kwa mitambo ya kuchoronga 15 kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Katika kongamano hilo, Mavunde aliwatangazia wachimbaji na wafanyabiashara kuhusu kupandishwa hadhi kituo cha ununuzi wa dhahabu cha Katoro kuwa soko kamili la dhahabu Katoro.

Wabunge wawili wa mkoa wa Geita, Joseph Musukuma na Tumaini Magesa, walimpongeza Rais Samia kwa kukuza uchumi wa wananchi wa Geita kupitia sekta ya madini kwa kujengewa mazingira rafiki ya ukuaji.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella aliahidi kwamba mkoa utaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia upatikanaji wa leseni 5.308 na mitambo ya uchorongaji.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages