
Baadhi ya vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi billioni mbili vilivyotolewa na shirika la Maji Safi Group kwa vituo tisa vya huduma za afya, ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Rorya na Shirati KMT jana.
-----------------------------------------
Shirika lisilo la kiserikali la Maji Safi Group limekabidhi kwa serikali ya wilaya ya Rorya, mkoani Mara msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi takriban bilioni mbili, kwa ajili ya kusambazwa kwa vituo tisa vya kutolea huduma za afya.
Mkurugenzi wa Maji Safi Group, Rachel Stephen na Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Dkt. Bwire Chirangi, walikabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Halfan Haule, katika hafla iliyofanyika kwenye kitongoji cha Sokorabolo jana.

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Halfan Haule (kulia), akipokea sehemu ya vifaa hivyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Safi Group (kushoto), Dkt. Bwire Chirangi na Mkurugenzi wa shirika hilo, Rachel Stephen.
-----------------------------------------
"Vifaa tiba hivi vimegharimu shilingi takriban bilioni mbili za kitanzania, kwa hiyo ni matumaini yetu kwamba vitachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa wilaya ya Rorya, hasa katika huduma za dharura na afya ya uzazi ya mama na mtoto," alisema Rachel.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya, Dkt. Haule, ambaye aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, Kanali Evans Mtambi, kwenye hafla hiyo, alielekeza vifaa hivyo vikabidhiwe kwa kamati za wananchi zinazosimamia vituo husika vya afya na vitumike kwa kazi iliyokusudiwa.
"Lazima tuvilinde vifaa hivi kwa kuzingatia mfumo wa ulinzi wa vifaa vya serikali, Kwa hiyo tukitoka hapa vikabidhiwe kwenye kamati za afya za msingi kwenye vituo vya kutolea huduma, lakini pia tupate taarifa ya mapokezi kutoka kwenye kila kituo kilichopokea vifaa hivi," alisema.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalfani Ilekizemba, alishukuru Maji Safi Group akisema vifaa hivyo vitaboresha zaidi kazi iliyoanzishwa na serikali.
Mkazi wa kitongoji cha Sokorabolo, Geofrey Matinde, alisema: "Tunawashukuru sana Maji Safi Group kwa msaada wanaotupatia, wametuletea maji kwenye zahanati yetu ya Sokorabolo na leo wametupatia vifaa hivi ambavyo vitaboresha huduma zaidi.”
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Maji Safi Group, Rachel Stephen, vituo vitakavyonufaika na msaada huo ni Hospitali ya Wilaya ya Rorya, Hospitali ya Shirati KMT, vituo vya afya Kinesi, Utegi, Changuge, zahanati za Sokorabolo, Nyamagaro, Nyambori na Rwang'enyi.

Mkurugenzi wa Maji Safi Group, Rachel Stephen, akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo. (Picha zote na Mara Online News)
-------------------------------------
Maji Safi Group ni shirika lisilo la kiserikali ambalo linatoa elimu ya afya, usafi wa mazingira, matumizi ya maji safi na salama pamoja na shughuli za kilimo katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mara.
No comments:
Post a Comment