
Mbunge wa Rorya, Jafari Chege.
Na Mwandishi Maalumu
KATIKA kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, utekelezaji wa Ilani ya chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM) umezaa matunda chanya katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na jimbo la Rorya.
Miradi mbalimbali ya kijamii iliyotekelezwa ndani ya jimbo la Rorya mkoani Mara katika kipindi hicho, ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya Rais Samia ya kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege, ameendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii katika jimbo hilo kwa kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.
Kupitia usimamizi wake makini na ushirikiano wa karibu na serikali pamoja na wana-Rorya, miradi ya maji, afya, elimu na barabara imeendelea kupewa kipaumbele cha kujengwa na kuboreshwa katika jimbo hilo.
Kwa mujibu wa Mbunge Chege, uongozi wa Rais Samia umefungua fursa mpya za maendeleo vijijini, huku akiendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote inayolenga kuinua hali ya maisha ya wakazi wa Rorya.
Sekta ya maji
Moja ya changamoto sugu katika jimbo la Rorya ilikuwa ni upatikanaji wa maji safi na salama. Kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia, miradi kadhaa ya maji imetekelezwa na mingine inaendelea kutekelezwa.
Miradi hiyo inajumuisha kufufuliwa kwa miradi ya maji, Komoge, Nyarombo, Nyambori, Sudi, Shirati, Nyihara, Ng’ope, Marasibora, Nyabimori na Masonga, bila kusahau ujenga wa miradi ya maji Rabour, Raranya, Kwibuse, Bukura, Gabimori, Nyanduga, Sakawa/ Mariwa na Muhundwe.
“Vilevile, upanuzi wa miradi ya maji Komuge, Kirogo, Makongro na Oliyo, usambazaji wa maji Shirati - Ingri Juu, Dett, Ochuna – Chereche – Mori, na ujenzi unaoendelea wa mradi mkubwa wa kusambaza maji Rorya – Tarime, ambapo kata zote 26 za Rorya zitanufaika,” alisema Chege katika mahojiano maalum na Mara Online News wilayani Rorya juzi.
Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuwezesha maelfu ya wananchi kupata huduma ya uhakika ya maji safi na salama, ambapo wanawake na watoto watapunguziwa adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Ni matarajio ya wengi kwamba miradi hiyo pia itasaidia kupunguza magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo safi na kuongeza muda wa wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Sekta ya afya
Hali kadhalika, Mbunge Chege anashuhudia kwamba katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, pia sekta ya afya jimboni Rorya imepewa msukumo mkubwa.
Anasema ni katika kipindi hicho ambacho umeshuhudiwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Rorya, vituo vya afya Nyamagaro na Rabour, zahanati za Kisumwa na Nyihara, ukamilishaji wa zahanati za vijiji vya Oliyo, Muhundwe, Ng’ope, Makongro, Manira na Dett, pamoja na upanuazi wa zahanati za Kogaja na Ikoma.
Utekelezaji wa miradi hiyo umeboresha upatikanaji wa huduma za afya za kiwango cha juu, zikiwemo za upasuaji na za mama na mtoto.
Zaidi ya hayo, serikali imeongeza idadi ya watumishi wa afya, ikiwemo madaktari na wauguzi, jambo ambalo limeimarisha utoaji wa huduma kwa wakati na kwa ufanisi.
Sekta ya elimu
Miundombinu ya elimu nayo imepewa kipaumbele katika jimbo la Rorya chini ya Ilani ya CCM na Serikali ya Rais Samia, ili kuwezesha watoto na vijana kupata elimu bora na jumuishi.
Mbunge Chege anataja miradi ya elimu iliyotekelezwa katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya za sekondari Mkengwa, Mika, Nyang’ombe, Nyamagaro, Ikoma, Rwang’enyi, Kisumwa, Kowak, Ingri Juu na Kinesi B.
Miradi mingine ni ujenzi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Rorya, ukamilishaji wa shule za sekondari mpya Nyambogo, Changuge na Kigunga, ujenzi wa shule mpya shikizi za Kanu na Obolo, na ujenzi wa vyumba vya madarasa 178 kutokana na fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
“Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Rais Mhe. Dkt. Samia kwa kutoa fedha za kufanikisha miradi hii ya elimu - ambayo itawapunguzia wanafunzi wa Rorya adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule,” anasema Chege.
Pia, upatikanaji wa madawati, vifaa vya kujifunzia na kuajiriwa kwa walimu wapya utachangia kuinua kiwango cha ufaulu, hasa kwa shule za kata. Haya yote yanadhihirisha dhamira ya serikali ya kuhakikisha elimu bora kwa kila mtoto bila kikwazo cha miundombinu.
Miundombinu ya barabara
Miundombinu ya barabara ni mhimili muhimu wa maendeleo ya uchumi na kijamii. Serikali imeonesha jitihada kubwa katika kufanikisha uboreshaji wa barabara muhimu katika jimbo la Rorya.
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, umeshuhudiwa ujenzi wa madaraja ya Mto Mori, Wamaya, Sakawa, Kabwana Michere na kivuko katika kijiji cha Mariwa jimboni Rorya.
“Pia, ufunguzi wa barabara mpya zenye urefu wa kilomita 168, utoboaji wa barabara kutoka Mbatamo hadi Isanga na kuimarisha barabara ya Nyamagaro – Kirogoro,” anaongeza Mbunge Chege.
Kwa niaba ya wananchi wa Rorya, Mbunge Mbunge anaishukuru Serikali ya Rais Samia pia kwa kuidhinisha ujenzi wa barabara ya Utegi – Shirati – Kirongwe kwa kiwango cha lami.
“Barabara hii kwetu ni muhimu sana kiuchumi, kibiashara na hata ukuaji wa pato la taifa kwa serikali itakapokamilika,” anasema mbunge huyo kutoka chama tawala - CCM.
Kwa mujibu wa Chege, ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umekuwa ukisubiriwa kwa miaka mingi, na kwamba ukitekelezwa utaboresha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika jimbo hilo.
Hivi karibuni, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia ilitangaza tenda ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kuanza na awamu ya kwanza ya Utegi - Shirati (kilomita 27).
Ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara umeongeza kasi ya biashara ndogo ndogo, usafirishaji wa mazao, pamoja na kuwezesha wananchi kuzifikia huduma za kijamii kama afya na elimu kirahisi.
Kwa hiyo, utekelezaji wa Ilani ya CCM katika jimbo la Rorya haujasalia kuwa maneno kwenye karatasi, bali umechukua sura ya miradi halisi na mageuzi ya maisha ya wananchi.
Kupitia uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, dira ya maendeleo imeendelea kufanikishwa kwa ushahidi wa huduma bora za maji, afya, elimu na barabara katika jimbo la Rorya.
No comments:
Post a Comment