
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha akizungumza na wananchi eneo la Nyaligongo ulipo mgodi wa dhahabu ilipotokea ajali iliyoua wachimbaji wadogo sita na kujeruhi wengine 11 juzi Jumamosi Mei 17, 2025.
-------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
Wachimbaji wadogo sita wamefariki dunia na wengine 11 kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na kifusi katika mgodi wa dhahabu uliopo Nyaligongo, Mwakitolyo mkoani Shinyanga.
Ajali hiyo ilitokea juzi Jumamosi Mei 17, 2025 saa 5:30 asubuhi, wakati wachimbaji hao wakiendelea na shughuli zao. Juhudi za uokoaji zilianza haraka, ambapo msaada mkubwa ulitolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, alifika mgodini hapo na kuthibitisha tukio hilo, akisema marehemu na majeruhi walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Mwawaza.
"Kikosi cha uokoaji kilikuwa tayari na mitambo 10 ya kisasa ya uokoaji lakini mitambo minne ilitosha kwa kazi hiyo iliyofanyika kwa ufanisi mkubwa," alisema Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro.

Sehemu ya mgodi huo ulioporomoka na kusababisha vifo vya wachimbaji wadogo sita na wengine 11 kujeruhiwa.
------------------------------------------
Mgodi huo ni kati ya migodi kadhaa inayoendesha shughuli za uchimbaji mdogo mdogo mkoani Shinyanga, na unamilikiwa na kikundi cha wachimbaji kiitwacho 'Hapa Kazi Tu'.
Serikali inaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo, sambamba na kuweka mikakati ya kuimarisha usalama na kuboresha mazingira katika shughuli za uchimbaji madini, hususan kwa wachimbaji wadogo mkoani Shinyanga.
No comments:
Post a Comment