NEWS

Monday, 19 May 2025

Mchango wa sekta ya madini kwa pato la taifa wapaa, wafikia asilimia 10.1



Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo picha) Mei 15, 2025 jijini Dodoma.
---------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Dodoma

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema sekta ya madini nchini imeendelea kupiga hatua kubwa, ambapo imekusanya maduhuli ya shilingi bilioni 902 sawa na asilimia 90.2 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni moja kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Mavunde aliyasema hayo Mei 15, 2025, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alieleza kuwa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa vilielekeza sekta ya madini ichangie asilimia 10 ya pato la taifa ifikapo mwaka 2025. Hata hivyo, tayari mwaka 2024 imefikia mchango wa asilimia 10.1, ikiwa ni mafanikio yaliyotangulia muda uliopangwa.

“Tumefanikiwa kuvuka lengo la kitaifa. Mwaka 2021 sekta ya madini ilichangia asilimia 7.3 kwenye pato la taifa, mwaka 2023 ilifika asilimia 9.1 na hivi sasa tupo kwenye asilimia 10.1 kufikia mwaka 2024. Hili ni jambo la kujivunia,” alisema Waziri Mavunde.

Aidha, maduhuli ya serikali kupitia sekta ya madini yameongezeka kwa asilimia zaidi ya 20 kutoka shilingi bilioni 623.24 mwaka 2021/2022 hadi bilioni 753.18 mwaka 2023/2024. Hadi kufikia Mei 9, 2025, Wizara ya Madini ilikuwa imekusanya shilingi bilioni 902, sawa na asilimia 90.2 ya lengo la mwaka.

Fedha za kigeni
Sekta ya madini imeendelea kuwa mhimili mkubwa wa upatikanaji wa fedha za kigeni. Mwaka 2023, mauzo ya madini nje ya nchi yalifikia dola za Marekani bilioni 3.55, yakichangia asilimia 46.1 ya mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi.

Aidha, kampuni za wazawa zimenufaika kwa kiasi kikubwa, ambapo bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.5 sawa na asilimia 92 ya thamani ya manunuzi yote migodini zilitolewa na Watanzania.

Kwa upande mwingine, sekta ya madini imezalisha ajira 19,356 katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023, ambapo kati ya hizo, ajira 18,853 sawa na asilimia 97.4 ni Watanzania.

Masoko na minada
Waziri Mavunde aliongeza kuwa serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuimarisha mazingira ya biashara ya madini kwa kuongeza idadi ya masoko na vituo vya ununuzi hadi kufikia 152 nchi nzima. Aidha, minada ya madini ya vito imeanzishwa upya baada ya kusimama tangu mwaka 2017.

Mnada wa kwanza ulifanyika Desemba 2024 na wa pili Aprili 2025, ambapo madini yenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 yaliuzwa na kuiwezesha serikali kukusanya shilingi milioni 163 kupitia mrabaha, ada za ukaguzi, usimamizi na ushiriki wa minada hiyo.

Vision 2030
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amesema utekelezaji wa Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri unaendelea kwa kasi. Maono hayo yanalenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za madini, kuongeza upatikanaji wa taarifa za jiosayansi, hususan za kina za jiofizikia na kuhakikisha sekta ya madini inaunganishwa kikamilifu na sekta nyingine kama viwanda, kilimo, fedha na ujenzi kwa ajili ya uchumi shirikishi na endelevu.

Programu ya MBT
Aidha, kupitia programu ya Mining for Brighter Tomorrow (MBT), serikali inatekeleza mpango mahsusi kwa ajili ya kuwainua wachimbaji wadogo, hususan wanawake na vijana kwa kuwapatia maeneo ya kuchimba na kuwasaidia teknolojia za kurahishisha shughuli zao.

Katika kuwajengea mazingira bora wachimbaji wadogo, serikali imefuta leseni na maombi 2,648 ambayo hayakuendelezwa na ina mkakati wa kuzigawa upya kwa wachimbaji wadogo.

Aidha, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeendelea kuwalea wachimbaji hao kupitia vituo vya mfano na mitambo ya CIP, huku kamati maalum ya watu sita ikiundwa kwa ajili ya kuishauri serikali kuhusu njia bora za kuwawezesha wachimbaji hao.

Pia, mfumo wa dhamana (Credit Guarantee Scheme) umeandaliwa sambamba na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuchakata chumvi kwa ajili ya kusaidia wakulima wa chumvi nchini.

Thamani ya madini
Kwa upande wa kuongeza thamani ya madini, Waziri Mavunde alisema, serikali inaendelea kuimarisha viwanda vya usafishaji, ambapo hadi sasa kuna viwanda tisa vya kuchakata madini ya metali kama shaba na nikeli, kikiwemo kiwanda kikubwa cha kusafisha makinikia cha Kbanga Nickel kinachojengwa eneo la Buzwagi mkoani Shinyanga, ambapo sita kati ya hivyo, vikitarajiwa kujengwa Dodoma.

Vilevile, ujenzi wa jengo la ghorofa nane la Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) unaendelea jijini Arusha kwa ajili ya kuongezea thamani madini ya vito.

Mafanikio mengine
Pia, katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. Samia, jumla ya leseni za uchimbaji mkubwa, wa kati na mdogo 34,348 zimetolewa na kampuni mbalimbali zimesaini mikataba kwa ajili ya kuanza uendelezaji wa migodi nchini.

STAMICO nalo limepiga hatua kubwa, kutoka kutengeneza faida ya shilingi bilioni hadi kufikia bilioni 84 kwa mwaka ndani ya miaka mitatu.

Mafanikio hayo ni taswira chanya ya sekta ya madini, ikiwa ni uthibitisho wa usimamizi na miongozo inayohakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali madini, jambo linaloifanya Tanzania kusimama imara kama moja ya nchi zenye mifumo madhubuti ya usimamizi na ukuaji wa sekta ya madini barani Afrika na kuvutia mataifa mengine kuja kujifunza hapa nchini.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages