NEWS

Monday, 19 May 2025

Wanafunzi 44 wahitimu Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kwa mwaka 2025



Wahitimu wa Mafunzo ya Ufundi ngazi ya Tatu (NVA level 3) katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime (TVTC) mjini Tarime wakiwa katika picha ya pamoja wiki iliyopita. Chuo hicho kinamilikiwa na Taasisi ya Professor Mwera (PMF).
-------------------------------------

NA JOSEPH MAUNYA, Tarime

WANAFUNZI 44 wamehitimu mafunzo ya ufundi ngazi ya Tatu (NVA level 3) katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime (Vocational Training College - TVTC) mwaka huu wa 2025.

Mahafali ya pili ya wahitimu hao wa mafunzo ya ufundi ngazi ya Tatu (NVA level 3) yalifanyika chuoni hapo wiki iliyopita.


Mgeni rasmi akikata utepe kuzindua 
sherehe za mahafali hayo.
--------------------------------------

Mkuu wa TVTC, Maria Daniel Tarimo, alisema wahitimu hao 44 ni kati ya wanafunzi 300 waliojiunga na chuo hicho mwaka 2022 kujifunza fani tofauti tofauti.

"Wahitimu hawa walijiunga na chuo chetu mwaka 2022 kwa ngazi ya level one katika kozi tofauti wakiwa 300, mpaka leo wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mtihani wa mwisho level 3 ni hawa 44 waliopo mbele yako leo," alisema Maria.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Ziwa, CPA Janet Nyoni, ambaye aliwataka wahitimu hao kuzingatia na kutumia vyema ujuzi na taaluma mbalimbali walizopata chuoni hapo.

"Mmetoka Tarime VTC, kwa hiyo mkawe mabalozi wazuri kwa kutumia kikamilifu ujuzi na elimu mliyopata chuoni hapa, pia jihadharini na makundi na tabia mbaya ili mjiepushe na majanga kama magonjwa ya kuambukiza, uraibu wa dawa za kulevya na kadhalika," alisema CPA Janet.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Professor Mwera Foundation (PMF) inayomiliki chuo hicho, Hezbon Peter Mwera, mwaka 2019 taasisi hiyo ilianzisha mpango wa kusaidia vijana wa Tarime kupata mafunzo chuoni hapo bure na kwamba tayari vijana zaidi ya 1,000 wamenufaika.

Mkurugenzi Hezbon akizungumza 
katika mahafali hayo.
--------------------------------------

Mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Ziwa, CPA Janet Nyoni (katikati waliokaa), viongozi mbalimbali na wahitimu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime (TVTC) wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa magahali hayo.
-----------------------------------------

Chuo hicho kinatoa mafunzo ya fani tofauti zikiwemo za ufundi magari, umeme, mabomba, uhazili, udereva, ushonaji, uongozaji watalii na upishi, miongoni mwa nyingine.

Wakati huo huo, Hezbon Peter Mwera ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa - kwa niaba ya umoja huo alomkabidhi Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Ziwa, CPA Janet Nyoni, tuzo ya pongezi kwa kazi nzuri anayofanya.

"Tuzo hii ni ya kukupongeza kwa kazi nzuri unayofanya kwa sababu kupitia kazi yako unapambana na maadui wakubwa ambao ni ujinga, maradhi na umaskini, pia sasa hivi tuna adui mwingine ambaye ni utandawazi ambaye anaweza kumpoteza mtu asipokuwa makini," alisema Hezbon.

Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, Hezbon Peter Mwera (kushoto), akimkabidhi Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Ziwa, CPA Janet Nyoni, tuzo ya pongezi kwa kazi nzuri anayofanya.
------------------------------------------

Hezbon alibainisha kuwa tuzo hizo zinazodhaminiwa na Professor Mwera Foundation hutolewa kwa viongozi mbalimbali ili kutambua umuhimu wa kazi zao katika jamii na kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa viongozi waliopewa tuzo hiyo.

Kwa upande wake, CPA Janet aliushukuru Umoja wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa kwa kumpatia tuzo hiyo ya heshima, huku akiwashukuru viongozi wa serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mafunzo ya ufundistadi nchini.

"Asante sana kwa tuzo hii ya heshima mliyonipatia, shukurani nyingi nizipeleke kwa viongozi wangu wanaoniongoza kufanya kazi hii, lakini pia rais wetu ambaye ndiye kiongozi anayesimamia elimu ya ufundi stadi nchini na hela nyingi ametoa kwa ajili ya ujenzi wa vyuo na vifaa vya kujifunzia," alisema.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages