
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Mohamed Shariff, akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo.
--------------------------------------------
Na Godfrey Marwa, Musoma
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara imefanikiwa kuzuia malipo hewa kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 70, kati ya hizo, milioni 49.2 zikiwa za kulipa makaburi hewa 123 katika kata ya Nyatwali wilayani Bunda ili kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Mohamed Shariff, ameyasema hayo leo Mei 27, 2025 wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita katika mkutano na waandishi wa habari mjini Musoma.
"Baada ya kufanya uchunguzi tulibaini makaburi hewa yasiyokuwa na mili (mabaki) ambapo kila kaburi lilitakiwa kulipwa shilingi 400,000, tukazuia malipo hayo kwani hayakuwa na sifa ya kulipwa fidia," amesema Shariff.
Ameongeza kuwa makaburi hayo yaliingizwa kwenye mfumo wa malipo wakati wa mchakato ufanyaji tathmini ambapo wahusika walionesha maeneo matupu, au matuta kuwa ni makaburi.
Katika hatua nyingine, Shariff amesema TAKUKURU imeokoa shilingi zaidi ya milioni 21 ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa awamu ya pili - ilihali vilikuwa tayari vimeishanunuliwa katika ujenzi wa awamu ya kwanza.
"Tulifanya uchunguzi na kubaini vifaa vilivyopangwa kununuliwa vilikuwa vimeishanunuliwa na vingine vilikuwa vimefungwa kwenye majengo husika wakati wa utekelezaji wa mradi awamu ya kwanza," amesema.
Kwa upande wa utekelezaji miradi, Mkuu huyo wa TAKUKURU ameeleza kuwa kwa kipindi hicho cha miezi mitatu miradi 28 yenye thamani ya shulingi zaidi ya bilioni tisa ilifuatiliwa na kuchunguzwa na kubainika kuwa na kasoro mbalimbali na kutoa ushauri katika sekta ya afya, elimu, barabara na maji.
"Kati ya miradi hiyo tulibaini kasoro na dosari kwenye miradi 12 yenye thamani ya shilingi bilioni 3.9 na kutoa ushauri ili marekebisho yafanyike kabla ya miradi hiyo kukamilika," amesema.
No comments:
Post a Comment