
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mangucha wilayani Tarime wakifurahia pichaya pamoja wakati wa tamasha la kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike lililoandaliwa na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Right to Play leo Mei 27, 2025.
----------------------------------------
Na Joseph Maunya
Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la Right to Play limeendelea na kampeni ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike kupitia shule za msingi katika wilaya za Tarime na Serengeti, mkoani Mara.
Wilayani Tarime kampeni hiyo imefanyika leo Mei 27, 2025 kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mangucha katani Nyanungu kupitia tamasha la michezo, ambapo Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo, ameihamasisha jamii kuachana na mila potofu dhidi ya watoto wa kike zinazowanyima haki ya kupata elimu.

"Leo tuko hapa Mangucha kuwambia wanajamii wote mlioko hapa kwamba muachane na zile mila potofu kama ukeketaji maana zinawazuia watoto wa kike kwenda shule, kwa sababu wanaweza kuvuja damu nyingi, na wengine wakishakeketwa wanaona wamekuwa wakubwa wanakimbilia kuolewa na kuacha shule," amesema Fungo.

Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo,
akizungumza katika tamasha hilo.
------------------------------------------
Kwa upande wake, Eliza Mwera Chacha ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Mangucha, amesema "Nimefahamu madhara ya ukeketaji kwetu watoto wa kike, kwa hiyo nawashauri wazazi pia wawe wanahudhuria matamasha haya ili nao wajifunze zaidi."
Tamasha lingine la kiuhamasishaji juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike lilifanyika Ijumaa Mei 23, 2025 kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Natta-Bigo iliyopo kata ya Natta, wilayani Serengeti.
Afisa Maendeleo wa Kata ya Natta, Tecla Itambiko, alipongeza AICT na Right to Play kwa kuandaa tamasha hilo akisema lina umuhimu mkubwa kwa maendeleo yao na jamii nzima.

Katika matamasha hayo ya kiuhamasishaji, mbali na michezo na burudani, pia taasisi hizo zimekuwa zikitoa zawadi mbalimbali kwa shule, ikiwa ni pamoja na vifaa vya michezo kama vile jezi na mipira, na vinywaji baridi kwa wanafunzi.
Kwa mujibu wa Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo, kampeni hiyo inaendeshwa chini ya mradi unaojulikana kama Serve Her Seat (Linda Kiti cha Mtoto wa Kike) kupitia matamasha ya michezo kwenye shule za msingi za wilaya za Serengeti na Tarime mkoani Mara.

No comments:
Post a Comment