
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akionesha Tuzo Maalum ya Heshima aliyotunukiwa na Bunge jana Jumamosi jijini Dotoma.
-----------------------------------------
Na Mwandishi Wetu
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutunukiwa Tuzo Maalum ya Heshima iliyotolewa na Bunge.
Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, alikabidhiwa tuzo hiyo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, katika hafla maalum iliyofanyika jijini Dodoma jana.
“Tuzo hii ni ushahidi wa wazi wa kuthaminiwa kwa uongozi wake madhubuti, unaojengwa juu ya misingi ya amani, maridhiano ya kisiasa, mshikamano wa kitaifa na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kwa Watanzania.
“Ni matokeo ya utekelezaji wenye mafanikio makubwa ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025 chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Aidha, tunajivunia kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kudhihirisha uimara, umakini na weledi wa chama katika kutoa uongozi thabiti kwa nchi yetu. Ni Fahari kwa CCM kuwa na kiongozi mwenye maono, uthubutu na dira ya maendeleo jumuishi kwa wote.
“Chama Cha Mapinduzi na wanachi wapenda maendeleo na amani nchini, tunamhakikishia Mheshimiwa Rais ushirikiano wa dhati, mshikamano usiotetereka na uungaji mkono mkubwa wakati wote anapotimiza wajibu wake kwa Watanzania.
“CCM ina imani kubwa na uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuliongoza taifa letu kwa amani, ustawi na mafanikio ya kweli,” ilieleza sehemu ya pongezi zilizotolewa na chama hicho tawala jana.
Bunge lilivyomuenzi Rais Samia
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemuenzi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumtunuku Tuzo Maalum ya Heshima - kama ishara ya kutambua na kuthamini uongozi na mchango wake katika kuleta maendeleo ya kisekta nchini.

Rais Samia (kulia) akipokea tuzo hiyo kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson.
------------------------------------------
Tukio hilo limeacha alama ya kipekee katika historia ya Tanzania, likiwa ni kielelezo cha kuthamini jitihada kubwa za Rais Samia katika kujenga taifa lenye ustawi, mshikamano na maendeleo endelevu.
Tuzo hiyo imeongeza orodha ya tuzo na heshima lukuki ambazo Rais Samia ametunukiwa na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi, kutokana na uongozi bora na mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Rais Samia aliwahusisha Watanzania wote katika heshima hiyo, akisema kuwa mafanikio ya serikali ni matokeo ya mshikamano, upendo, ushirikiano na uzalendo uliooneshwa na wananchi pamoja na viongozi katika kipindi chake cha uongozi.
Aidha, Rais Samia alilipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuisimamia serikali kwa weledi kupitia mijadala ya bajeti, kupitisha sheria muhimu na kutoa ushauri wenye tija kwa serikali.
Alieleza kuwa mchango wa Bunge hilo umesaidia kwa kiwango kikubwa katika kuboresha utendaji kazi wa serikali katika ngazi zote.
Hafla ya kumkabidhi Rais Samia tuzo hiyo ilihudhuriwa na viongozi tofauti wa serikali, wabunge na wananchi mbalimbali waliokusanyika kushuhudia tukio hilo la kihistoria - lililobeba uzito wa kitaifa na heshima kwa kiongozi mkuu wa nchi.
No comments:
Post a Comment