NEWS

Saturday, 31 May 2025

CCM yazindua Ilani ya Uchaguzi ya 2025-2030, Rais Samia asema yaliyomo yanatekelezeka



Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (wa nne kushoto mbele) na viongozi mbalimbali wakionesha vitabu vya Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya Mwaka 2025-2030 iliyozinduliwa jana Mei 30, 2025 jijini Dodoma.
------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua rasmi Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2025-2030 wakati kikihitimisha Mkutano Mkuu Maalum wa siku mbili, huku kikibainisha idadi ya wanachama wake inayofikia milioni 13.

Uzinduzi huo ulifanyika jijijini Dodoma jana Mei 30, 2025, ukiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Ilani ya CCM, Prof. Kitila Mkumbo, alisema imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi na dira ya maendeleo ya taifa.

Prof. Kitila alisema Ilani hiyo imebeba vipaumbele tisa, ikiwamo kuboresha maisha ya watu, kuimarisha ustawi wa jamii, na kuendelea kupunguza umaskini nchini.

“Vipaumbele vingine ni kuchochea mapinduzi ya kisiasa yaliyo jumuishi, shindani na fungamanishi, kuongeza thamani ya rasilimali za ndani na kupanua fursa za ajira kwa vijana na kuongeza kipato cha wananchi,” aliongeza.

Kwa mujibu wa ilani hiyo, serikali ya CCM itatengeneza ajira milioni nane ndani ya miaka mitano ijayo katika sekta rasmi na isiyo rasmi nchini.

Ilani hiyo imezingatia pia kuharakisha maendeleo maeneo ya vijijini ambako pamoja na mambo mengine, mkazo utaelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.

Hivyo, ilani hiyo inatarajiwa kuwa nyenzo kuu ya kampeni za CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo chama hicho tawala kinalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika awamu zilizopita.

CCM kimekuwa chama cha kwanza kuzindua ilani yake wakati joto la Uchaguzi Mkuu ujao likiwa bado halijashika kasi kutokana na mazingira ya kisiasa yanayoshuhudiwa wakati huu, hasa baada ya chama kikuu cha upinzani - CHADMA kutishia kutoshiriki uchaguzi huo, kikishinikiza mageuzi katika vyombo vya utendaji, ikiwamo katiba na sheria.

Chama hicho tawala kinazindua ilani yake huku kikijivunia ongezeka la idadi ya wanachama wake waliofikia milioni 13 waliosajiliwa kwa mfumo wa kidigitali.

Wakati wa uzunduzi wa ilani hiyo, wagombea urais wa Tanzania wa CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgombea wake mwenza, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, pamoja na mgombea urais wa Zanzibar, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, walikabidhiwa ilani na kisha kuzionesha kwa wajumbe kuashiria utayari wao wa kwenda kuzinadi kwa wananchi wakati wa kampeni.

Rais Samia akizungumza wakati wa ufungaji wa mkutano huo, alisema yaliyomo kwenye ilani hiyo yanatekelezeka. "Tushawishi watu watuunge mkono, waungane nasi katika kuitekeleza ilani hii," alisema.

CCM imehitimisha mkutano wake mkuu maalum, huku ikiwa imepitisha pia marekebisho madogo ya katiba ambayo yanakaribisha mageuzi ya kidigitali na kuongeza idadi ya wajumbe katika baraza la wadhamini.

Kama ilivyo ada ya CCM, mkutano wake huo ulihudhuriwa pia na vyama rafiki vya ukombozi vya kusini mwa Afrika, Watanzania wanaoishi nje ya nchi wakiwemo kutoka Uingereza na Marekani, jumuiyaya wafanyabiashara na wasanii kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma, miongoni mwa wageni waalikwa wengine.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages