NEWS

Thursday, 19 June 2025

Yametimia Mwanza: Rais Samia azindua Daraja la JP Magufuli “Kigongo Busisi” Ziwa Victoria



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Daraja la JP Magufuli "Kigongo-Busisi katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza leo Alhamisi Juni 19, 2025.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Alhamisi Juni 19, 2025 amezindua rasmi Daraja la kimkakati la JP Magufuli katika Ziwa Victoria linalounganisha maeneo ya Kigongo wilayani Misungwi na Busisi wilayani Sengerema, mkoani Mwanza.

Ujenzi wa daraja hizo lenye urefu wa kilomita 3.2 na maungio yake, umegharimu shilingi zaidi ya billion 700 kutoka serikalini.

Rais Samia amewasili mkoani Mwanza leo mchana akitokea mkoani Simiyu ambako alikuwa na ziara ya siku kadhaa ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi mbalimbali wakitembea juu ya Daraja la JP Magufuli "Kigongo-Busisi".
----------------------------------------

Mara baada ya kuwasili kwenye Daraja la JPM, Rais Samia amekata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa daraja hilo ambalo ni la kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki na Kati na la sita kwa ukubwa Afrika nzima - lililojengwa kwa technolojia ya kisasa kabisa.

Baada ya kusomewa historia fupi ya mradi wa ujenzi huo ulioanza miaka mitano iliyopita, Rais Samia ameshuhudia magari ya kwanza yakipita katika daraja hilo, ambapo alipungiana mikono na abiria waliokuwa kwenye magari hayo - wakionesha bashasha kubwa kwa nafuu kubwa ya usafiri watakayoanza kuipata kwa kutumia miundombinu hiyo.

Baadaye Rais Samia amehutubia taifa kupitia mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi katika eneo hilo la kimakakati.

Katika hotuba yake, Rais Samia amesema wakati anaingia madarakani mwaka 2021 alipokea ujenzi wa daraja hilo ukiwa asilimia 25.

Amesema daraja hilo lina umuhimu mkubwa kwa mikoa ya Mwanza, Kagera na Kigoma, ambapo wananchi watakuwa wanatumia dakika nne kuvuka kwa gari.

“Lengo limetimia. Daraja hili litakuwa alama kwa nchi yetu… ni fahari nyingine kubwa kwa nchi yetu. Tunauona mwanga wa dhana ya kujitegemea,” amesema Rais Samia na kueleza faraja yake kuzindua daraja hilo.

Aidha, kiongozi huyo wa nchi amesisitiza kuwa daraja hilo ni la kimkakati, hivyo mamlaka husika hazina budi kulilinda, kulitunza na kulifanyia ukaguzi mara kwa mara.
Sambamba na Rais Samia, viongozi karibu wote wakuu wa kitaifa wamehudhuria hafla hiyo, akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania (Bara), Stephen Wasira, Mjane wa Mwasisi wa ujenzi wa daraja hilo, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Janeth, mawaziri mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, miongoni mwa wengine.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages