
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (aliyevaa miwani), akishirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (katikati), kukabidhi mizinga 143 ya kufugia nyuki kwa wazee wazee wa mila kutoka koo 12 za kabila la Wakurya wilayani humo jana. (Picha na Mara Online News)
------------------------------------------
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime mkoani Mara, Meja Edward Gowele, amewakabidhi wazee wa mila kutoka koo 12 za kabila la Wakurya wilayani humo mizinga 143 ya kufugia nyuki iliyotolewa na ofisi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Lengo la kuwapa mizinga hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 9.5 ni kuunga mkono juhudi za wazee hao katika kulinda mazingira, ikiwemo mistu, kujipatia kipato kwa kuuza asali, kudumisha amani na kukomesha migogoro.
"Ninyi ni wahifadhi wakubwa wa mazingia kwenye maeneo yenu, tumechangia mizinga 143 kwa ajili yenu wazee kwa kushirikiana na vijana wenu," alisema Meja Gowele wakati wa makabidhiano hayo ambayo baadaye yalihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, mjini Tarime jana.
"Tunachoomba mtusaidie kutatua migogoro katika jamii, kudumisha amani kwenye maeneo yetu, kuombea Uchaguzi Mkuu ufanyike kwa amani na utulivu," aliongeza.

Katibu wa Baraza la Wazee hao, Mwita Nyasibora, alishukuru akisema mizinga hiyo itawasaidia kulinda misitu dhidi ya uvamizi, kujipatia kipato kwa kuuza asali na kuhifadhi mazingira muhimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Aidha, wazee hao walimshukuru na kumuombea Meja Gowele maisha marefu wakisema viongozi wengi wamepita Tarime lakini hawakufanya tukio la aina hiyo. “Tunashukuru migogoro mingi ameitatua,” alisema mmoja wa wazee hao.
No comments:
Post a Comment