NEWS

Wednesday, 30 July 2025

Sababu za Nyambari Nyangwine kupewa nafasi kubwa kinyang’anyiro cha ubunge Tarime Vijijini


Nyambari Nyangwine

Na Mwandishi Maalumu

Jumanne ya Julai 29, 2025, chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliingia rasmi katika hatua muhimu ya mchujo mwingine wa ndani kwa ajili ya kuwapata wagombea wake wa nafasi za ubunge kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiuwa kufanyika nchini Oktoba 29, 2025.

Miongoni mwa majina yaliyoibua mjadala mkubwa na matumaini mapya katika jimbo la Tarime Vijijini, ni Nyambari Nyangwine - mwanasiasa mwenye historia ya mafanikio, mbunifu, mzalendo wa kweli na mwenye maono makubwa ya maendeleo ya wananchi.

Ushawishi wake

Uteuzi wa Nyambari kugombea kura za maoni ndani ya CCM za ubunge katika jimbo la Tarime Vijijini haujaja kama mshangao kwa wengi, kwani kwa miaka kadhaa, amekuwa akihusishwa na siasa safi, za kujenga na zenye msukumo wa maendeleo ya watu.

Anaelezwa kuwa na ushawishi mkubwa kwa wajumbe wa kura za maoni kutokana na ukaribu wake nao, uwezo wake wa kusikiliza changamoto zao na dhamira ya kusaidia kuzitatua.

Katika mikutano ya ndani na shughuli mbalimbali za chama, Nyambari amekuwa akionesha uwezo mkubwa wa kujenga hoja, kushirikiana na viongozi wa ngazi zote na kuhamasisha umoja na mshikamano wa wana-CCM.

Nyambari anatajwa na wengi kuwa ni mtu wa watu - anayefahamika kwa upole, uadilifu, uaminifu, busara, hekima, unyenyekevu na msimamo thabiti katika kusimamia rasilimali za umma.

Maono ya maendeleo

Kinachomtofautisha Nyambari Nyangwine na wagombea wengine wengi ni namna anavyoliangalia jimbo la Tarime Vijijini kisera na kimaendeleo.

Kwa kutaja maendeleo machache aliyofanikisha, Nyambari wakati akiwa mbunge alishirikiana na viongozi wengine kuweka msukumo uliowezesha jimbo la Tarime kugawanywa kuwa majimbo mawili ya uchaguzi, yaani Tarime Mjini na Tarime Vijijini.

Lakini pia, ndiye mbunge pekee mwenye rekodi ambayo haijawahi kuvunjwa ya kushirikiana na wazee wa mila hadi kufanikiwa kukomesha mapigano ya kikoo katika wilaya ya Tarime.

Zaidi ya hayo, Nyambari ndiye mbunge pekee ambaye aliweza kuomba mabati 6,000 kutoka TANAPA na kuyagawa wilaya nzima ya Tarime kwa ajili ya kuezeka majengo ya shule na vituo vya kutolea huduma za afya.

Kama kawaida yake, Nyambari amekuwa akitamani kuona miradi ya kijamii, ikiwemo elimu, afya, maji, barabara, umeme na mawasiliano inaimarishwa kwa ustawi wa wananchi.
Nyambari Nyangwine

Katika mawasiliano yake na wananchi, amekuwa akisisitiza kuwa Tarime Vijijini inahitaji kiongozi mwenye uwezo wa kupanga, kutekeleza na kusimamia ajenda za maendeleo kwa vitendo - si kwa maneno matupu.

Nyambari anaamini katika matumizi sahihi ya rasilimali, ushirikishwaji wa jamii katika maamuzi na ubunifu katika kutatua changamoto sugu kama vile ukosefu wa ajira kwa vijana na hali duni ya huduma za kijamii.

Kupitia uzoefu wake katika siasa, Nyambari ambaye amepata kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mwaka 2010-2015, amejijengea uwezo wa kuunganisha sekta binafsi na serikali katika kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Mvuto kwa wananchi
na uungwaji mkono

Upepo wa kisiasa unazidi kuvuma kwa kasi upande wa Nyambari. Mikusanyiko ya wananchi, mitandao ya kijamii na vikao vya kisiasa visivyo rasmi vinaendelea kutawaliwa na mazungumzo kuhusu nafasi yake na kile anachoweza kukifanya akipewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao.

Wananchi wengi wanamwelezea Nyambari kama kiongozi mwenye historia ya kutenda na mwenye uwezo wa kusimamia kwa uwazi, uadilifu na uaminifu mkubwa masuala yenye maslahi kwa wananchi kwa ustadi na weledi mkubwa.

Uwezo wake wa kujieleza, kusoma alama za nyakati na kuelewa mwelekeo wa kisera wa kitaifa ni sifa zinazomfanya aonekane kuwa chaguo sahihi kwa wakati huu.

Wadau mbalimbali, wakiwemo wazee wa mila, viongozi wa dini, vijana na wanawake, wanaonesha matumaini makubwa kwamba Nyambari amekuja na nguvu mpya ya kuliongoza jimbo la Tarime Vijijini kwa mafanikio makubwa iwapo atapitishwa na chama na baadaye kuchaguliwa na wananchi.

Katika uchaguzi wa ndani, CCM ina nafasi ya kufanya maamuzi yatakayoakisi dhamira yake ya kweli ya kuwatumikia wana-Tarime Vijinini. Kupitia uteuzi wa wagombea wenye uwezo, maono na weledi, chama kinaweza kujiongezea mvuto kwa wananchi na kuimarisha nafasi yake katika Uchaguzi Mkuu.

Nyambari Nyangwine ambaye pia ni mfanyabiashara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, ni mzalendo wa kweli anayelenga kuona Tarime Vijijini ikipiga hatua kubwa za maendeleo endelevu ya kisekta.

Kama chama kitaamua kumpitisha, wananchi nao watakuwa na nafasi ya kufanya uamuzi wa hekima - kumpa mtu mwenye dira, nguvu na nia ya kweli ya kuwawakilisha kikamilifu bungeni na kuwatumikia wananchi wa jimbo la Tarime Vijijini kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages