NEWS

Monday, 28 July 2025

Ilani ya CCM 2020-2025 ilivyotekelezwa kwa mafanikio makubwa kata ya Rabuor wilayani Rorya chini ya uongozi wa Ng’ong’a



Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan 
na Gerald Samwel Ng'ong'a (GSN).
---------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu

Hakika wana-Rabuor hawakukosea kuchagua kiongozi wao. Ndivyo tunaweza kuelezea uongozi wa Gerald Samwel Ng’ong’a (GSN), Diwani wa Kata ya Rabuor tangu mwaka 2020 kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye baadaye alichaguliwa na madiwani wenzake kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, mkoani Mara.

Leo hii, wananchi wa Rabuor wanashuhudia mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025, ambapo katika kipindi cha miaka mitano, miradi ya kijamii inayogusa moja kwa moja maisha yao imetekelezwa kila kona ya kata hiyo chini ya uongozi wa Ng’ong’a.

Kijiji cha Makongro
Historia ya maendeleo ya kata ya Rabuor haiwezi kuandikwa bila kutaja kijiji cha Makongro, ambapo uongozi wa Ng’ong’a umeking’arisha kwa miradi ya kijamii, kama vile ujenzi wa boma la choo katika Shule ya Msingi Kasino uliogharimu shilingi 700,000 kutoka mfuko wake binafsi.

Miradi mingine iliyotekelezwa kijijini Makongro chini ya uongozi wa Diwani Ng’ong’a, ni ujenzi wa chumba cha darasa katika Shule ya Msingi Kasino kilichogharimu shilingi milioni 12.5 na ujenzi wa matundu ya vyoo vya wanafunzi kwa gharama ya shilingi milioni 24 kutoka serikalini.

Aidha, Ng’ong’a anasema alitoa fedha zake binafsi kiasi cha shilingi 760,000 kugharimia ujenzi wa choo kingine cha wanafunzi katika Shule ya Msingi Kasino, lakini pia alitoa shilingi 360,000 zilizogharimia upanuzi wa nyumba ya mwalimu katika shule hiyo.

Pia, ujenzi wa choo cha walimu Shule ya Msingi Kasino uliogharimu shilingi 603,000, jiko na stoo Shule ya Msingi Kagecha kwa gharama ya shilingi 6,000,000, jiko na stoo Shule ya Msingi Kasino kwa shilingi 6,017,000, jiko na stoo Shule ya Msingi Ligero (shilingi 5,651,000) na chumba cha darasa Shule ya Msingi Kagecha (shilingi milioni 13), zote hizo kutoka mfuko binafsi wa Ng’ong’a.

Vilevile, Diwani Ng’ong’a alijitolea kununua matofali 800 na nondo nane vilivyogharimu shilingi 4,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa boma Shule ya Msingi Kagecha na sare za shule za watoto wenye uhitaji maalum katika shule zote saba zilizopo kata ya Rabuor kwa gharama ya shilingi 1,000,000.

Zaidi ya hayo, Ng’ong’a alitoa shilingi milioni 13.59 zilizogharimia ujenzi wa bweni la kisasa katika Shule ya Sekondari Odunga, huku serikali nayo ikitoa shilingi milioni 30 zilizogharimia ujenzi wa maabara katika shule hiyo.

Katika kipindi hicho pia serikali ilitoa shilingi milioni 12.5 zilizogharimia ukamilishaji wa chumba cha darasa katika Shule ya Sekondari Odunga, shilingi 8,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa choo, shilingi milioni 500 zilizogharimia ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Rabuor na shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Makongro.

Serikali pia ilitoa shilingi 1,438,000 zilizogharimia upakaji rangi na kufunga mfumo wa maji katika Zahanati ya Makongro, lakini pia shilingi 700,000 kwa ajili ya matengenezo ya madirisha matatu ya vyoo katika zahanati hiyo.

Maendeleo mengine yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Ng’ong’a ni ujenzi wa choo cha walimu Shule ya Sekondari Odunga kwa gharama ya shilingi 500,000 zilizotolewa na diwani huyo, pamoja na uchimbaji wa lambo Ligero (shilingi 3,000,000).

Ng’ong’a anataja miradi mingine iliyotekelezwa kipindi chake cha uongozi kuwa ni ukarabati wa barabara ya Nyayo-Kasino kwa gharama ya shilingi milioni 50 na ujenzi wa jengo la Kituo cha Polisi Kasino kwa shilingi 3,590,000 zilizotolewa na diwani huyo.

Kijiji cha Oliyo
Kijijini Oliyo nako miradi mingi imetekelezwa, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa vyumba vitatu vya madarasa Shule ya Msingi Oliyo B kwa gharama ya shilingi milioni 2.2 na ukarabati wa ofisi ya Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Oliyo A kwa shilingi 900,000 zilizotolewa na Ng’ong’a.

Ujenzi wa msingi wa chumba cha darasa Shule ya Msingi Oliyo A kwa shilingi 470,000, ujenzi wa choo cha walimu kwa shilingi 590,000 na ununuzi wa madawati 10 kwa ajili ya shule za msingi Oliyo A na B kwa shilingi 1,000,000 zilizotolewa na Ng’ong’a.

Miradi mingine iliyotekelezwa katika kijiji hicho kwa mujibu wa Diwani Ng’ong’a, ni ujenzi wa anamu ya jengo la utawala Shule ya Sekondari Oliyo (shilingi 300,000), chumba cha darasa na matundu kadhaa ya vyoo vya wanafunzi katika shule hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 27.3 kutoka serikalini.

Miradi ya maji nayo haikuachwa nyuma kwani Ng’ong’a alitoa shilingi 70,000 zilizogharimia ukarabati wa kisima cha Shule ya Msingi Oliyo B, huku serikali ikitoa shilingi milioni 50 zilizogharimia ukarabati wa barabara ya Buturi-Maduki-Oliyo Lami.

Vilevile, serikali ilitoa shilingi milioni 50 zilizogharimia ukamilishaji wa Zahanati ya Kijiji cha Oliyo, huku Diwani Ng’ong’a akitoa shilingi milioni 3.899 kugharimia ujenzi wa choo Shule ya Msingi Oliyo B na shilingi 100,000 kulipia bima za afya kwa kaya tano zisizojiweza.

Ng’ong’a anasema pia alinunua mtungi wa gesi kwa shilingi 120,000 kwa ajili ya huduma za Zahanati ya Kijiji cha Oliyo, huku shilingi milioni 50 zilizotolewa na serikali zikigharimia ujenzi wa barabara ya Oliyo-Kagecha na shilingi milioni 12.5 zilitumika kugharimia ukarabati wa chumba cha darasa Shule ya Msingi Oliyo A.

Kijiji cha Rabuor
Kama ilivyo katika vijiji vya Makongro na Oliyo, maendeleo makubwa yameshuhudiwa pia katika kijiji cha Rabuor, ukiwemo ukarabati wa chumba cha darasa na anamu Shule ya Msingi Mariwa kwa shilingi milioni 1.5.

Lakini pia, ujenzi wa choo cha walimu Shule ya Msingi Mariwa kwa shilingi 540,000, ununuzi wa madawati 10 kwa ajili ya shule za msingi Mariwa na Buturi kwa shilingi 1,000,000 zilizotolewa na Ng’ong’a, na mabati ya shilingi milioni 1.8 kutoka serikalini yaliyoezeka baadhi ya majengo ya Shule ya Msingi Mariwa.

Kwa upande mwingine, serikali ilitoa shilingi milioni 4.8 zilizogharimia ujenzi wa jiko na stoo Shule ya Msingi Buturi, shilingi 400,000 zilizotolewa na Diwani Ng’ong’a ambazo ziligharimia ukarabati wa nyumba ya mwalimu Shule ya Sekondari Buturi na shilingi milioni nne kutoka serikalini ziligharimia utengenezaji wa madirisha ya grill ya bwalo la chakula Shule ya Sekondari Buturi.

Diwani Ng’ong’a alitumia shilingi milioni 7.5 kutoka mfuko wake binafsi kununua kompyuta tano na printer moja kwa ajili ya Shule ya Sekondari Buturi, huku serikali ikitoa shilingi milioni 20 zilizotumika kugharimia ujenzi wa chumba cha darasa katika shule hiyo.

Miradi mingine iliyotekelezwa katika kijiji cha Rabuor katika kipindi cha uongozi wa Diwani Ng’ong’a ni ujenzi wa bweni, vyumba vitano vya madarasa na matundu saba ya vyoo, vyote hivyo vikigharimu shilingi milioni 269.7 kutoka serikalini.

Aidha, katika hatua ya kupambana na njaa shuleni, Diwani Ng’ong’a alitoa mahindi magunia 10 na kuyagawa kwenye shule zote za katani Rabuor, na kwa upande mwingine serikali ilitoa shilingi milioni 49.65 zilizogharimia ujenzi wa Zahanati ya Buturi.

Diwani Ng'ong'a (katikati) akikabidhi msaada wa mahindi magunia 10 kuchangia chakula cha wanafunzi shuleni.
---------------------------------------------

Pia, shilingi milioni 600 zilitolewa na serikali kugharimia uchimbaji wa kisima kikubwa cha kusambaza maji kwa wakazi wa vijiji vyote vitatu vinavyounda kata ya Rabuor [Makongro, Oliyo na Rabuor], huku ukarabati wa skimu ya Rabuor ukivunja rekodi kwa kugharimu shilingi bilioni moja zilizotolewa na serikali.

Miradi mingine ni ufunguaji wa barabara ya Makongeni-Mariwa kwa gharama ya shilingi milioni nane, ukarabati wa kisima cha Ong’ayo kwa shilingi 220,000 zilizotolewa na Ng’ong’a, na ujenzi wa nyumba pacha ya watumishi wa afya kwa shilingi milioni 28.6.

Ng‘ong’a wa maendeleo
Katika kipindi cha miaka mitano tu, Gerald Ng’ong’a ameandika historia ya maendeleo makubwa katani Rabuor. Kila kijiji kimeguswa, huku sekta za elimu, afya, maji ba barabara zikipewa kipaumbele.

Chini ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025 ambayo imekuwa dira ya maendeleo ya kisekta, Diwani Ng’ong’a ameonesha kuwa uongozi si maneno matupu bali ni utekelezaji wa ahadi kwa vitendo.

Katika kata ya Rabuor, maendeleo hayazungumzwi tena - yanaonekana. Miradi mingi ya kijamii imeshuhudiwa ikitekelezwa kwa ufanisi katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Ng’ong’a ambaye anatajwa na wakazi wa kata hiyo kama kiongozi wa maendeleo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages