NEWS

Saturday, 26 July 2025

Wakurugenzi Mara wapokea kompyuta 142 kuimarisha mfumo wa kidijitali vituo vya huduma za afya



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi (kushoto), akikabidhi kompyuta kwa mnoja wa wakurugenzi wa halmashauri ili kuimarisha mfumo wa GoTHOMIS kwenye vituo vya huduma za afya.
--------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, amekabidhi kompyuta 142 kwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, miji na manispaa zilizotolewa na Wizara ya Afya ili kuimarisha mfumo wa mawasiliano wa GoTHOMIS kwenye vituo vya huduma za afya mkoani humo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo mjini Musoma jana, Kanali Mtambi aliwataka wasimamizi wa sekta ya afya kuhakikisha matumizi ya mfumo huo yanafika asilimia 100 katika mkoa huo.

Kwa mujibu kiongozi huyo, awali mkoa wa Mara ulikuwa unashika nafasi ya kwanza kwa ufungaji na matumizi ya mfumo huo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, ila kwa sasa umeshuka baada ya mikoa mingine kuongeza jitihada.

“Sasa mhakikishe tunarudi kwenye nafasi yetu ya awali, na hii inawezekana baada ya kupata msaada huu ambao unaenda kutatua changamoto ya ukosekanaji wa vifaa katika vituo vya kutolea huduma za afya,” aliagiza.

Alisema kwa sasa mkoa huo hauna sababu ya kuendelea kubaki kwenye asilimia 90 ya matumizi ya mfumo wa GoTHOMIS, hivyo aliitaka Divisheni ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kuhakikisha kuwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinafunga na kutumia mfumo huo.
Aidha, Kanali Mtambi alitoa muda hadi Agosti 30, 2025 vituo vyote vya kutolea huduma za afya mkoani Mara viwe vimefungwa mfumo wa GoTHOMIS na kuzitaka divisheni za afya, lishe na ustawi wa jamii za halmashauri kusimamia matumizi sahihi ya kompyuta hizo.

Kwa upande mwingine, kiongozi huyo wa mkoa alikemea tabia ya watumishi wa sekta ya afya kuchelewesha huduma kwa wananchi kwa kisingizio kuwa mfumo unasumbua, kumbe wanataka kutoa huduma nje ya mfumo - jambo ambalo alisema linasababisha wizi wa fedha za serikali.

“Watumishi ambao hawaujui vizuri mfumo au matumizi ya kompyuta wajifunze na kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuboresha utendaji wao na kutoa huduma bora kwa wananchi bila visingizio,” alisema kanali Mtambi.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya, alisema kompyuta hizo zitausaidia mkoa huo katika kuimarisha matumizi ya mfumo wa GoTHOMIS ambao unadhibiti mapato ya serikali katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Kusaya aliongeza kuwa matumizi ya mfumo huo yakiimarisha yatawezesha pia mawasiliano kuboreshwa kati ya vituo vya kutolea huduma za afya na taasisi mbalimbali za serikali.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Divisheni ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, Dkt. Zabron Masatu, aliishukuru Wizara ya Afya kuupatia mkoa wa Mara kompyuta hizo, na kuahidi kuwa zitatumika kama ilivyokusudiwa.

“Vifaa hivi vitasaidia kuboresha upatikanaji wa vifaa katika matumizi ya mifumo mbalimbali ya afya ili kutuwezesha kudhibiti mapato ya serikali na utoaji wa taarifa kwa wakati,” alisema Dkt. Masatu.

GoTHOMIS ni mfumo wa kidijitali uliobuniwa na serikali – ambao unawezesha ufuatiliaji wa huduma, utunzaji wa taarifa, takwimu za wagonjwa, mapato ya fedha na dawa kwa urahisi, na kutoa ripoti sahihi kwa wakati ili kuchochea ufanisi na maendeleo ya huduma za afya nchini.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages